Jeshi la polisi mkoa wa singida linawashikilia mwalimu Regina Laurent (28) wa shule ya msingi Mang’onyi na Mathias Marmo(30) wote Wairaq na wakazi wa Mang’onyi kwa tuhuma za kumuua kwa kipigo mtoto mwenye umri wa miaka mitano(5) aitwaye Joyce John ,mkazi wa kijiji na kata ya Mang’onyi ,wilayani Ikungi mkoani hapo.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa polisi mkoa wa singida kamishna msaidizi wa polisi (ACP) Stella Mutabihirwa amesema watuhumiwa hao walikuwa ni walezi wa mtoto na kwamba walipata taarifa ya tukio hilo siku ya agosti 11,2021 majira ya saa nane usiku baada ya wauguzi wa Hospitali ya Malkia wa Ulimwengu iliyopo maeneo ya Puma wilayani Ikungi mkoani Singida waliompokea mtoto huyo ambaye alifariki wakati akipatiwa matibabu kutilia mashaka kifo hicho kutokana na majeraha aliyokuwa nayo marehemu na ndipo wakaamua kutoa taarifa kwa jeshi la polisi.
Amesema uchunguzi wa awali ulibaini kuwa majeraha ya mtoto huyo yalitokana na kupigwa na vitu vilivyodhaniwa kuwa ni fimbo na kitu butu katika sehemu mbalimbali za mwili wake na kuwa watuhumiwa wameshakamatwa na uchunguzi zaidi ukikamilika wote wawili watafikishwa mahakamani kujibu shtaka linalowakabili.
Aidha ameongeza uchunguzi wa awali umebaini kuwa mtoto huyo alikuwa akifanyiwa ukatili mara kwa mara kwa kupigwa na walezi wake hao.
Baada ya uchunguzi wa kitabibu kukamilika mwili huo ulikabidhiwa kwa ndugu kwa hatua za mazishi .
Jeshi la polisi mkoani humo linaendelea kukemea vitendo vya kikatili vinavyofanywa na baadhi ya wazazi na walezi na kuwaomba kuachana na vitendo hivyo vikiwemo kutoa adhabu zisizo na mipaka kwa watoto na kuwaasa wananchi kuwalea watoto katika maadili mema
0 Comments