ABIRIA Treni ya Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (TAZARA )waliotoka Mkoani Mbeya stesheni ya Iyunga tangu Septemba 17,2021 Wamekwama katika stesheni ya TAZARA Makambako Mkoani Njombe huku wakidai kupata changamoto mbalimbali ikiwemo ya kushinda njaa kutokana na  kuishiwa fedha.            

Akizungumza mjini Makambako, abiria Bw.Rubeni Simchimba ,amesema alikata tiketi yeye na  watoto wake watatu ambao anawapeleka chuo Ifakara Mkoani Morogoro tangu Septemba 17 mwaka huu 2021 saa 3 asubuhi na ilipofika jioni wakataarifiwa kuwa warudi makwao hadi watakapojulishwa.

 "Mwandishi wa habari Mimi nilishtushwa na kauli hiyo natokea Mkoani Songwe Wilaya ya Momba mawasiliano yangu na  wenzangu watayapataje ? Amehoji Bw.Simchimba.
Nae Abiria mwingine Bi.Agnesi Mwabukusi kutokea Chimala Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya ,amesema yupo na Watoto wawili Wanakwenda Mang'ula Mkoani Morogoro lakini tangu jumamosi ameishiwa fedha za chakula na anaishi kwa kuwaombea maji Watoto wake kwa abiria wenzake na kufanya yeye na watoto wake waishi kwa maji ya kunywa ya kuomba kwa wasamaria wema.  
 Juhudi za kuwanusuru abiria hao hazikuzaa matunda  kutokana na Afisa aliyepatikana wa Makao makuu ya TAZARA Dar es salaam kutokuwa tayari kuzungumzia suala hilo kwa njia ya simu. 
Msimamizi wa Taasisi ya kutetea abiria  Tanzania (CHAKUA)mkoa wa Njombe Bw.Zulu Nyunza, amesema kinachofanyika ni ukiukwaji mkubwa wa haki za abiria na haki za msingi za binadamu,kwani  abiria kutelekezwa hapo nikutowatendea haki. 
"Mwandishi wa habari hapa stesheni master TAZARA Makambako angepatikana ilitakiwa ahakikishe  abiria waliofika Jana usiku saa 5 hadi saa 7:15 mchana ,asubuhi wamepata chai na mchana huu chakula na ikibidi ni lazima kuwatafutia usafiri mbadala wa mabasi kuelekea waendako siyo kuwaacha njia panda "  Bw.Nyunza.

Hata hivyo juhudi zinafanyika kuwasiliana na Wizara ya Uchukuzi ili kuona namna nzuri itakayofaa kuwasaidia abiria hao.