WATU wanne wamethibitika kupoteza maisha na wengine 33 kujeruhiwa baada ya basi la kampuni ya Fikosh lililokuwa likitoka mkoa wa Mwanza kuelekea mkoa wa Kagera kuacha njia na kupinduka katika mteremko wa Nyangoye ulioko katika manispaa ya Bukoba Mkoa wa Kagera. 

Akitoa taarifa ya ajali hiyo iliyotokea leo septemba 9,2021 .mkuu wa wilaya ya Bukoba Moses Machali amesema  basi hilo lenye namba za usajili T710 BXB wakati linapata ajali lilikuwa likitokea mkoa wa Mwanza na lilikuwa limebakiza umbali mfupi kuingia katika kituo kikuu cha mabasi cha Bukoba.

Machali amesema taarifa hizo ni za awali, na kwamba kama kutakuwa na ongezeko la vifo  au majeruhi watatoa taarifa baadae.

"Polisi wanaendelea na uchunguzi ili kujua  chanzo cha ajali na idadi ya abiria waliokuwemo, tunaomba subira taarifa rasmi itatolewa baadae ikikamilika" amesema Machali

Kamanda wa polisi mkoani Kagera Revocatus Malimi amethibitisha taarifa hiyo na kueleza kuwa miongoni mwa waliopoteza maisha watatu ni watu wazima na mmoja ni mtoto mdogo.

"Maiti zimepelekwa na kuhifanyiwa katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Kagera, na majeruhi wamepelekwa katika hospitali hiyo kwa ajili ya matibabu, uchunguzi unaendelea,  na taarifa za watu walioshuhudia wamedai gari hilo lilipoteza mwelekeo baada ya kumaliza kona katika mteremko huo na kuanguka pembezoni mwa barabaraba"