WATU Wasiofahamika wamechoma makanisa mawili (Kilokole) yaliyopo  Mtaa wa Namanyigu kata ya Mshangano Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma na kusababisha hasara ya zaidi ya shilingi milioni moja kufuatia samani zilizokuwepo kwenye makanisa hayo.

Mchungaji Alfred Milanzi wa kanisa la Pentekoste Tanzania (KLPT) amesema kuwa tukio hilo limefanyika Septemba sita majira ya saa kumi alfajiri baada ya majirani waliopo karibu na kanisa hilo kupiga kelele kuwa kanisa linaungua moto.

Milanzi amesema kufuatia kelele hizo alitoka na kwenda kusaidiana na majirani kuuzima  moto huo lakini vitu  na samani mbalimbali vilivyokuwa kanisani humo vimeteketea kwa moto .

Amesema  wakati wakiendelea kuzima moto kanisani hapo wakasikia tena kelele kwenye kanisa lingine kuwa linaungua moto ambalo ni kanisa la Tanzania Carval Teberenakuro ambayo yapo jirani kwenye mtaa huo na kuwa kanisa hilo limeshachomwa mara mbili mfululizo.

Makanisa hayo yaliezekwa kwa matrubai na waumini wamekuwa wakiabudia siku zote ,hivyo ameiomba Serikali iweze kuchunguza kwa kina kufuatia tukio hilo ili kufanikisha kukomesha vitendo hivyo.

Kwa upande wake mwenyekiti wa mtaa wa Namanyigu Abdulqadir Myao amesema Serikali ya mtaa kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi tayari wameshaanza kulifanyia kazi tukio hilo huku akilaani vitendo hivyo ambavyo amesema vinataka kuhatarisha amani na kuifanya jamii iwe na hofu isiyokuwa na sababu ya msingi.

Naye Askofu wa Kanisa la Pentekoste Tanzania Jimbo la Songea, Grayson Mapunda amesema vitendo hivyo havikubaliki na kuwa kanisa linaviachia vyombo vya dola viendelee na uchunguzi wa jambo hilo.

Kufuatia tukio hilo Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma , Joseph Konyo akizungumza kwa njia ya simu amesema kuwa tayari jeshi hilo linafanya upelelezi ili kuwabaini waliyohusika na vitendo hivyo.