Klabu ya Simba imesaini mkataba wa miaka minne na Kampuni ya uuzaji na ukodishaji magari ya Africarriers kwa ajili ya kuzisafirisha timu ikiwamo ya wakubwa, Wanawake (Simba Queens) na vijana chini ya umri wa miaka 17 wenye thamani ya Sh milioni 800.

Africarriers wametoa basi kubwa aina ya Golden Dragon la kisasa lenye uwezo wa kubeba abiria 60 kwa timu ya wakubwa, Eicher yenye uwezo wa kubeba watu 35 kwa ajili ya Timu ya Wanawake na Costa kwa ajili ya Timu ya Vijana.

Rasmi sasa Africarriers wanakuwa wasafirishaji wa timu tatu za Simba kwa njia ya barabara kama ilivyo kwa Air Tanzania kwa njia ya anga.

Mkurugenzi wa Masoko wa Africarriers, Zain Pirbhai amesema kama moto wao unavyosema ‘We Drive Africa’ na Simba wanafanya vizuri kwenye michuano ya Afrika hivyo wanafurahia kufanya kazi nao.

Mtendaji Mkuu wa klabu, Barbara Gonzalez amesema jezi za timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17 itakuwa na nembo ya Africarriers kifuani wakati zile za kusafiria za wakubwa na zile za Simba Queens zitakuwa na nembo hiyo mkononi.