Mkurugenzi mtendaji wa Asasi ya Millenium Arts Group ,Mnung'a Mnung'a akizungumza na wakazi wa kata ya Magagura Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma, kuhusu elimu ya utawala bora na ufutiliaji wa Rasilimali za Umma(PETS)


   Na. Amon Mtega ,SONGEA.

WANANCHI wa kata ya Magagura Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma wametakiwa kutambua haki zao kwa kushirikishwa katika shughuli mbalimbali za utekelezaji wa miradi inayofanywa kwenye maeneo yao ili kuondoa baadhi ya malalamiko ambayo huwa yanatokea kwenye jamii.

Wito huo umetolewa na Mnung’a Mnung’a ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa Asasi isiyokuwa ya Kiserikali ya Millenium Arts Group yenye makao yake Wilaya ya Songea mkoani humo inayojishughulisha na utoaji wa elimu kwa wananchi juu ya ushirikishwaji wa miradi inayotekelezwa kwenye maeneo yao pamoja na elimu ya utawala bora na ufuatiliaji wa Rasilimali za umma(PETS).

Mnung’a akizungumza na mamia ya wakazi wa kata ya Magagura kwenye mkutano wa hadhara ambao umeandaliwa na Asasi hiyo ambayo inafadhiliwa na shirika la Foundation For Civil Society kutoka Dar es salaam amesema katiak maeneo mengi kumekuwa na migongano baina ya Wananchi na Viongozi wao ambayo inatokana na kutokuwa na ushirikishwaji katika kutekeleza miradi hiyo.

Mkurugenzi huyo amesema kuwa  kupitia Asasi hiyo imekuwa ikitoa elimu katika maeneo ya kata mbalimbali za Wilaya ya Songea ,ambapo hadi sasa wamezifikia kata nane ambazo ni Magagura,Kizuka,Litapwasi,Mpitimbi,Muhukuru barabarani,Lilahi,Peramiho na Litisha na kuwa mradi wa utoaji elimu hiyo unagharimu shilingi Milioni arobaini na tano(Tsh,45,000,0000=)kwa miezi nane kuanzia Agosti 2021 hadi Machi 2022.

 Amesema kuwa fedha nyingi za Serikali zimekuwa zikipelekwa kwenye kata hizo kwaajili ya kutekeleza miradi lakini kumekuwepo na baadhi ya Viongozi wa Vijiji na Kata kuzifanyia kinyume na malengo yaliyokusudiwa jambo ambalo limekuwa likirudisha nyuma jitihada za Serikali za kuwahudumia Wananchi wake.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Magagura , Christian Hyera akizungumza na wakazi wa Kijiji hicho kuwa ofisi yake itashughulikia changamoto za madai ya Wananchi hao.


Kwa upande wake mwenyekiti wa Kijiji cha Magagura Christian Hyera ameipongeza Asasi hiyo na kuwa yeye kama kiongozi ataitumia elimu hiyo vema ili wananchi waweze kuzitambua haki zao za msingi hasa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Hyera pia alitumia nafasi ya mkutano huo kujibu kero mbalimbali zilizoibuliwa na Wananchi hao baada ya kupatiwa elimu ya ushirikishwaji na utawala bora ambapo amesema atazifanyia kazi na kama kuna mwananchi hakutendewa haki na moja ya viongozi wa kwenye ofisi hiyo atalifanyia kazi.

Moja ya kikundi cha Sanaa kikitumbuiza kwenye mkutano na Wananchi wa kata ya Magagura wakati wa kupatiwa Elimu juu ya utawala bora .

Naye mmoja wa wananchi wa kata hiyo Sholastika Ndomba amesema Asasi hiyo imewapa elimu pana maana katika kata yao kumekuwepo  na baadhi ya changamoto ya kutokusomewa mapato na matumizi pamoja na baadhi ya michango ya maendeleo hutolewa bila kupatiwa stakabadhi (RISITI)jambo ambalo limekuwa likiibua maswali mengi kwa wananchi hao.

Katika utoaji elimu hiyo Asasi hiyo imekuwa ikitumia zaidi mfumo wa vikundi vya sanaa namna ya kufikisha ujumbe kwenye jamii jambo ambalo limewafanya wakazi wengi waweze kuwa na uelewa wa kutambua haki zao ikiwemo haki ya kushiriki mikutano toka ngazi za chini hadi juu.