WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa bilioni 2.469 kwa ajili ya kuvifanyia maboresho vituo 42 vya mizani nchini kikiwemo na kituo cha Mingoyo kilichopo eneo la Mnazi Mmoja kwenye barabara ya Mtwara-Mingoyo-Masasi mkoani Lindi .

Pia, Mheshimiwa Majaliwa ametoa muda wa miezi miwili kuanzia  Oktoba 5, 2021 hadi Novemba 30, 2021 uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi uwe umetenga eneo kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha mabasi na maegesho ya malori.

Ameyasema hayo Oktoba 5, 2021 wakati akizungumza na wananchi katika eneo la Mnazi Mmoja mkoani Lindi baada ya kukagua kituo cha Mizani cha Mingoyo akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika mkoa huo.