Na Amon Mtega, Ruvuma.

Maafisa Maendeleo ya jamii wa Halmashauri za Mkoani Ruvuma wametakiwa kuongeza viwango vya mikopo  kwenye makundi maalumu likiwemo la  wanawake wajasiriamali ili waweze kufikia malengo yaliokusudiwa.

Wito huo umetolewa na katibu tawala wa Wilaya ya Songea Upendo Daniel alipokuwa akifunga maonyesho ya biashara zinazoibuliwa na wanawake wa mkoa huo (Tanzania Women Chamber of Commerce).

Katibu tawala huyo ambaye alimuwakilisha mheshimiwa Jenista Mhagama Waziri wa Nchi ,Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera,Bunge ,Kazi,Vijana,Wazee ,Ajira na wenye ulemavu na mbunge wa Jimbo la Peramiho amesema wanawake wengi kwenye vikundi vyao vya biashara wanashindwa kufikia malengo waliokusudia  kutokana na changamoto ya kupatiwa mikopo midogo kutoka kwenye Halmashauri zao.

Akizungumza kwenye uhitimishaji wa maonyesho hayo amesema  kama wanawake  wajasiriamali wakipatiwa mikopo mikubwa kidogo kuanzia sh,Milioni kumi(10) badala ya sh.Milioni mbili basi ndoto za wanawake huo zitafikiwa malengo ikiwemo uanzishwaji wa viwanda vidogovidogo vya kuzalishia bidhaa

“Katika hili niwatake maafisa maendeleo ya jamii kupitia Halmashauri zenu kwenda kujipanga upya namna ya utoaji wa mikopo kwenye makundi maalumu likiwemo la wanawake ambao wamekuwa kipaumbele katika kutumia fursa zilizopo mkoani Ruvuma .

Mwenyekiti wa wanawake Mkoani Ruvuma Rosemary Ngonyani wa kwanza kushoto akimuonyesha mgeni rasmi Upendo Daniel wapili kushoto  baadhi ya bidhaa zinazozalishwa na wakinawake hao.

Kwa upande wake mwenyekiti wa chama cha wanawake mkoani Ruvuma Rosemary Ngonyani awali akisoma risala mbele ya mgeni rasmi huyo amesema kuwa wanawake hao licha ya changamoto za mikopo lakini bado wamekuwa na changamoto ya masoko ya bidhaa zao kutokana na baadhi kutokuwa na mwamko wa kutumia bidhaa ya ndani.

Amesema kuwa hali hiyo imekuwa ikiwakatisha tamaa baadhi ya wanawake kuendelea kuwa na maono makubwa ya kuzalisha bidhaa zao kwa wingi zaidi.


Mjasiriamali Siwazuri Mwinyi akimuonyesha mgeni rasmi Upendo Daniel bidhaa wanazozalisha kwenye kikundi chao

Katika maonyesho hayo baadhi ya wajasiriamali akiwemo Siwazuri Mwinyi ambaye anatengeneza bidhaa na usambazaji wa bidhaa za Usafi na Vipodozi Asilia amewapongeza watu wa viwango (TBS)kuwa wamekuwa hawana urasimu katika kuwasaidia wajasiriamali wadogowadogo .

 Amesema kuwa tangu watu wa viwango wamuruhusu bidhaa zake zimekuwa na soko kubwa la ndani ya Nchi na Nje ya Nchi jambo ambalo limekuwa likimtia moyo katika ufanyaji kazi hiyo.

Wafanyakazi wa NSSF wakiwa wameshika cheti walichozawadiwa kufuatia mchango walioutoa kwa wanawake wa Mkoa wa Ruvuma.

Hata hivyo mwenyekiti huyo akisoma risala hiyo mbele ya mgeni rasmi huyo amesema mafanikio ya maonyesho hayo ya siku saba yamesaidiwa na wadau mbalimbali kutoka kwenye taasisi za watu binafsi  na za kiserikali kama NHIF ,NSSF na Redio Jogoo ambayo amesema ilirusha matangazo bure juu ya zoezi la maonyesho hayo.