MSD YAPEWA WIKI MOJA KUPELEKA DAWA KOTE NCHINI


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD) Meja Jenerali Gabriel Saul Mhidze ahakikishe mpaka kufikia Jumamosi, Oktoba 16, 2021 dawa ziwe zimepatikana katika maeneo yote nchini.

Waziri Mkuu amesema kuwa ni maelekezo ya Serikali kuwa vituo vyote vya kutolea huduma zikiwamo zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya, hospitali za rufaa za mikoa lazima zipate dawa kwa kuwa zinategemea MSD

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumapili, Oktoba 10, 2021) alipokutana na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin Mollel pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa MSD Meja Jenerali Gabriel Saul Mhidze.

“Utaratibu wa Serikali ni kuwa hatutaki kuona mwananchi anaenda kwenye maeneo ya kutolea huduma za afya na kuelekezwa kwenda kununua dawa katika maduka ya mtaani, Serikali inapeleka fedha kila mwezi, nimetoa hii wiki, sio Lindi tu ni pamoja na mikoa mingine yote nchini dawa lazima ziende, kazi yenu ni kuhakikisha dawa zinakwenda kwa kuwa fedha mnalipwa”

Aliongeza kuwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amesema anatoa tena fedha kwa ajili ya ujenzi hivyo ni lazima Serikali ipeleke dawa, vifaa na wataalamu.

Pia, Waziri Mkuu amewataka viongozi wa Taasisi hiyo wahakikishe wanapeleka malori 10 ya dawa katika kila kanda lengo ni kuwezesa upatikanaji wa dawa ili kurahisisha utoaji wa huduma.

Kadhalika Waziri Mkuu amemtaka Meja Jenerali Gabriel Saul kuhakikisha anaisimamia MSD na asisite kufanya marekebisho pale panapoonekana pana mapungufu. “Tunataka tuondoe malalamiko kwa wananchi kuhusu upatikanaji wa dawa, fedha ipo hakuna haja ya kuwepo kwa malalamiko”

Kwa upande wake, Meja Jenerali Gabriel ameahidi kusimamia utendaji kazi wa taasisi hiyo ili kuondoa dosari zote zinazokwamisha upatikanaji wa dawa katika vituo vyote vya kutolea huduma na atahakikisha mapungufu hayo hayatajirudia.

 

(mwisho)

 

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

JUMAPILI, OKTOBA 10, 2021.

Post a Comment

0 Comments