Diwani wa kata ya Likuyuseka Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma Kassim Gunda akionyesha miche ya miti asili inayooteshwa na kikundi cha mwamko kilichopo katani hapo.

NA AMON MTEGA,NAMTUMBO.

DIWANI wa Kata ya Likuyuseka Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma Kassim Gunda amekita kikundi cha Mwamko (Mwamko Group) kinachojishughulisha na uoteshaji wa miche ya Miti ya asili kwa ufadhili wa Kampuni ya Mantra Tanzania Limited kilichopo katani hapo kuotesha miche hiyo kwa wingi ili kuenda sambamba na malengo ya Serikali ya kupambana na uharibifu wa mazingira yanayo sababisha mabadiliko ya tabia Nchi.

Gunda ametoa wito huo wakati kampuni ya Mantra inayojishughulisha na madini ya Uranium katika mto Mkuju uliopo Wilayani humo kupitia Meneja uhusiano Khadija Pallangyo kwenda kukagua maendeleo ya uoteshaji wa miche hiyo kwenye kikundi hicho .


Akizungumza na wanakikundi hao diwani huyo amesema kuwa kampuni ya Mantra Tanzania Limited imetoa ufadhili wa mbegu za miti ya asili ili kuboresha mazingira yalioharibiwa hivyo ni vema wanakikundi hao wakaongeza jitihada ya kuotesha miche mingi ili mwisho wa siku kuendana sambamba na mpango wa Serikali wa kukabiliana na changamoto ya uharibifu wa misitu unaosababisha mabadiliko ya tabia Nchi.

Hata hivyo diwani Gunda ameipongeza kampuni ya Mantra Tanzania Limited kwa kuendelea kujitoa kwenye shughuli za kijamii kwa kutoa misaada mbalimbali katika sekta ya Uboreshwaji wa mazingira,Elimu,Afya na Michezo huku akiongeza kuwa suala la kuboresha mazingira atalisimamia kwa nguvu zote na kuhakikisha kila kwenye maeneo ya Shule na taasisi nyingine kwenye kata hiyo zinapanda miti ya asili ikiwemo na kwenye vyanzo vya maji.


Amesema siku za nyuma kumekuwa na dhana potovu kuwa miti ya porini haina sababu ya kupandwa kwa kuwa Mungu anaiotesha tu apendavyo jambo ambalo limepelekea kuharibiwa kwa mazingira ovyo na kusababisha mabadiliko ya tabia Nchi.

Meneja Uhusiano wa Kampuni ya Mantra Tanzania Limited Khadija Pallangyo wa pili kulia mwenye miwani akimsikiliza mwenyekiti wa kikundi cha mwamko Hassan Nihuka juu ya uoteshaji wa miche ya miti asili walivyoweza kufanikiwa baada ya Kampuni hiyo kuwafadhili pamoja na Wataalam walioenda kuwapa elimu.

Kwa upande wake meneja uhusiano wa kampuni ya Mantra Khadija Pallangyo amesema kuwa lengo la kukisaidia kikundi hicho mbegu za miti ya asili ni kutaka kuendelea kuyaboresha mazingira kwenye maeneo yaliyokatwa miti ya asili irudishiwe miti hiyo kwa kuipanda,ambapo hadi sasa zaidi ya Sh.2,000,000=(Milioni mbili).


Meneja uhusiano huyo amesema licha ya miche ya miti lakini bado wamefadhili mbegu za mboga za majani ili ziweze kulimwa kwa wingi kwa kutumia mbolea za wanyama (Samadi) pamoja na mbolea vunde ambayo tayari watalaam walienda kutoa elimu kwa wanakikundi hao namna ya kuitengeneza mbolea hiyo na kuachana na utumiaji wa mbolea za kemikali .

Mwenyekiti wa kikundi cha Mwamko Hassan Nihuka akizungumzia kuhusu uoteshaji wa miti asili unaofanywa na kikundi hicho kwa ufadhili wa Kampuni ya Mantra Tanzania Limited.

Naye mwenyekiti wa kikundi hicho Hassan Nihuka amesema kuwa hadi sasa wameotesha miche Elfu nane (8,000)malengo ni kutaka kufikisha miche zaidi ya Elfu thelathini (30,000) ili kukabiliana na changamoto ya uharibifu wa mazingira ambapo katika Wilaya hiyo asilimia kubwa umesababishwa na kilimo cha Tumbaku .


Nihuka ameishukuru kampuni ya Mantra kwa ufadhili huo lakini bado amesema kuwa kampuni hiyo imeweza kuwasaidia miche ya miti ya mitunda mbalimbali ikiwemo ya miparachichi ambayo tayari imeshaoteshwa.

Diwani wa Viti maalum wa Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma Dhamani Komba akiahidi kushirikiana na kikundi cha mwamko kilichopo kata ya Likuyu seka kinachootesha miti asili.

Pia naye diwani wa Viti maalum Dhamani Komba amekipongeza kikundi hicho ambacho ni cha kwanza katika ukanda wa kata hiyo kufanya kazi ya uoteshaji wa miche ya miti asili huku akiahidi kuwaunga mkono katika kuendeleza jitihada hizo.