MAMBO 5 MUHIMU YA KUZINGATIA KABLA HUJAAMUA KUOA/KUOLEWA


Ukiwa bado hujaoa au hujaolewa unaweza ukawa unapata ugumu wa kutambua mambo gani ya kuzingatia ili uwe na ndoa imara kutokana na wengi wetu kutokuwa na maarifa ya kutosha juu ya mahusiano.

Unaweza kupata ugumu wakati wa machaguo yako au wakati wa kufanya maamzi, hasa binti anaweza kukutana na changamoto hii akiwa amejiwa na wanaume Zaidi ya mmoja, wote wakiwa na lengo la kumwoa.

Vile vile kwa mwanaume inaweza ikawa changamoto kujua ni mwanamke gani au binti gani kati ya wale anaowaona au anaokutana nao anaweza akawa mke wake. Hasa kijana akiwa na hali nzuri kiuchumi na kiroho anaweza kupata changamoto Zaidi, maana mabinti wengi wanakuwa karibu naye.

Lengo la mabinti kuwa naye karibu ni kujionyesha kuwa wanafaa kuolewa naye, utakuwa shahidi kama umeona kijana wa kiume kabla ya kuoa alikuwa na marafiki kadhaa wa kike ila baada ya kuoa au kuchumbia wale mabinti waliondoka, na wengine huwa wanahama na kanisa.

Unaweza ukaona ni jinsi gani ilivyo na ugumu kidogo kujua nani anaweza akawa mwenzi wangu sahihi wa maisha, hasa ukiwa huna maarifa ya kutosha inaweza kukusumbua sana na unaweza ukapitia maumivu ya kuacha na kuachwa.

Katika somo hili tutajifunza mambo machache na muhimu ya kuweza kukusaidia katika kuweza kufanya maamuzi sahihi;

Yafuatayo ni mambo muhimu ya kuzingatia kabla ya kufanya maamuzi ya kuoa/kuolewa;

1. Awe Ameokoka

Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza? 2 Wakorintho 6:14

Hii ni sifa muhimu sana kwa muoaji au muolewaji yeyote, ukiwa kama kijana uliyempokea Yesu kama Bwana na mwokozi wa maisha yako hupaswi kupuuza jambo hili. Unaweza kupata rafiki asiyeokoka na wewe ukawa umeokoka ukajipa matumaini kuwa utaenda kumfanya aokoke ukiwa kwenye ndoa, utapata shida na kuchukia ndoa.

Kama unatamani aokoke, vizuri ukamhubiri akaokoka kabla ya kuingia naye kwenye ndoa, ikiwa utashindwa kumfanya aokoke kabla ya ndoa uwe na uhakika hata ukiwa ndani ya ndoa hutamuweza kirahisi.

Unapaswa kufahamu kwamba sisi huwa hatubadilishi watu, anayeweza kubadilisha mtu ni Yesu mwenyewe, sasa kama Yesu hatambadilisha mkiwa wachumba au marafiki unategemea mkiingia kwenye ndoa ataenda kumbadilisha? Lazima utafakari hili kwa usalama wako.

2. Mwenye Bidii Ya Kazi

Hii sifa unaweza usielewe sana kwa sasa ila ni muhimu sana, ndoa nyingi zinaingia kwenye migogoro kwa sababu unakuta mke ni mvivu wa kazi, au mume ni mvivu wa kazi. Hataki kujishughulisha na kazi yeyote, anapenda awe amekaa tu nyumbani, au awe anadhurura.

Nafsi ya mtu mvivu hutamani asipate kitu; Bali nafsi ya mwenye bidii itanenepeshwa. Mithali 13:4.

Mtu mwenye bidii ya kazi atafanikiwa, hata kama leo unamwona hana kitu kikubwa sana ila kadri anavyojibidisha katika kazi atapata mali. Ukiwa na mume mwenye bidii huwezi kuwa mtu wa kulala njaa, mvua ikinyesha ataenda kulima, mtapata mazao mtakula.

Ukiwa na mume/mke mwenye bidii na kazi huwezi kukaa nyumba ya kupanga miaka yote hadi unazeeka, maana atakuwa mpambanaji na mtasaidiana mengi katika ndoa yenu. 

Sasa ukiwa unataka kuoa/kuolewa na mtu ambaye unaona leo hana mali unazotoka, usiogope kuoa/kuolewa naye kama anajibidisha na kazi mtaenda kuzipata mkiwa kwenye ndoa yenu. Maana mtaenda kuzitafuta mkiwa pamoja kwenye ndoa, kama unaona hili huliwezi vizuri ukafanya maamzi mapema. Usije ukawa mwiba kwa mwenzako, maana kila siku utakuwa unamhoji kwanini hana pesa za kutosha.

3. Mwenye Upendo Wa Kweli

Wengi huwa tunavutiwa na vitu vya kawaida kabisa hasa uwezo wa mtu kifedha, mwanaume/mwanamke anaweza kukupenda kwa sababu una mali, akiwa anatazamia kuwa hatopata shida mkiwa kwenye ndoa. Sasa hapa kuna hatari hii, anaweza kuwa amependa tu mali zako ila sio wewe, huyu atakupa shida sana maana macho yake yatakuwa kwenye mali zako.

Mbaya Zaidi huwa wanategeneza mahusiano mengine ya nje, maana kwako anakuwa hana ule upendo wa kweli ila kilichomsukuma awe na wewe ni hizo fedha zako au mali zako. Utashangaa vituko anavyovifanya kwako, na utaanza kulalamika anakosa nini kwako, ujue ni zile hisia za upendo kwako anakuwa hana.

Sisemi kuwa na fedha za kutosha ni vibaya, na simaanisha wenye pesa wote au wenye mali wote wana matatizo la hasha! Hapa napenda kukufungua ufahamu kuwa mali zisiwe ndio kigezo cha wewe kumpenda na kumwoa binti au kuolewa na mwanaume.

Mnaweza mkawa na mali nyingi sana ila mwenzako akawa hana upendo na wewe, utalia kila siku na pesa zipo ndani za kutosha, elewa pesa sio kipimo cha kuishi maisha ya furaha ndani ya ndoa yako. Bali pesa ni sehemu tu ya kuwasaidia kupata mahitaji muhimu ya kimwili.

4. Misingi Ya Imani Yenu IweMoja(Ifanane)

Kuna madhehebu yanabatiza kwa maji machache na mengine maji mengi, kama wewe unaamini ubatizo wa maji mengi na ukaolewa au ukaoa mwenzako anayeamini ubatizo wa maji machache. Uwe na uhakika itawaletea shida kwa watoto wenu, wewe utataka watoto wako wabatizwe kwa maji mengi, na mwenzako atataka wabatizwe kwa maji machache tena wakiwa wachanga.

Wengine wanaamini kupiga makofi ni dhambi, ukioa au ukiolewa na mtu wa namna hiyo unaweza kuja kupata shida maana wewe utataka mwenzako apige makofi atakataa, au wewe utapiga makofi mwenzako atakwazika. Utataka watoto wako wapige makofi mwenzako atawakataza kupiga.

Wengine wakataza kusuka, utatamani mke wako awe anasuka na kwenda salon kutengenezwa vizuri ila mwenzako atakuwa anaona kufanya hivyo ni dhambi, hii ni kujitengenezea mgogoro usio wa lazima ndani ya ndoa yako. 

Mgogoro kama huu unaweza kuepukana nao mapema kabla ya kufanya maamzi ya kuingia kwenye mahusiano ya ndoa na unayemwona anaweza akawa mume/mke wako. Ama anaweza akakubali muwe dhehebu moja kabla ya kuingia kwenye ndoa ili akupate, ila mkishaingia kwenye ndoa anarudi alipokuwa anasali.

Nimeona baadhi ya ndoa zikiwa zinapata shida hapa, unakuta mume anasali RC na mke anasali FPCT inapofika siku ya jumapili watoto wanaanza kupata changamoto, mama anataka watoto waende anaposali, na baba naye anataka watoto waende anaposali. Chanzo cha misuguano huanza hapo, inatoka kwa watoto inaingia kwa wanandoa wenyewe.

5. Tabia Kuendana

Haiwezekani kufanana kila kitu, hata biblia inaposema “msaidizi wa kufanana na wewe” haimanishi kila kitu, yapo madhaifu unayo, Mungu atakupa wa kuweza kukusaidia katika eneo hilo. Ukipata wa sawa yako atakuchukulia hayo madhaifu yako na wengine wa nje wanaweza wasiyaone hayo maana tayari yupo anayeziba hilo pengo.

Kuwa na muda wa kumfahamu vizuri mwenzako, zile tabia usizozipenda mweleze mapema, kama anaweza kubadilika uone mkiwa hamjaingia kwenye ndoa. Ukiona hataki kubadilika na wewe unaona huwezi kubeba huo mzigo bora kumwacha mapema, usilazimishe moyo wako, ukiulazimisha utaenda kuteseka, maana utakuwa umechukua mke sio wako au utakuwa umechukuliwa na mume asiye wako.

Kuna msemo mmoja wa Kiswahili unasema hivi “ndege wanaofanana huruka pamoja” usije ukajichanganya ukaingia kwenye mahusiano na mtu unayeona kuna mambo mengi hamuendani naye. Utakuja kufa siku sio zako, tumekua kwenye familia tofauti, zipo familia zenye uwezo wa juu kiuchumi na kielimu, na zipo familia za uchumi wa chini na elimu ya kati. Utajipa shida wewe na familia yako, wakati mwingine utakuwa unajiona kunyanyapaliwa kutokana na hali yako ya chini kiuchumi.

Mwisho, msikilize sana Roho Mtakatifu, yapo mambo mengine kibinadamu tunaweza kuona sio sawa ila wewe kama wewe Mungu anaweza akawa amezungumza na wewe. Hapa Mungu kuzungumza na wewe uwe makini sana, maana shetani naye hujifanya malaika wa nuru, atakuja kuzungumza na wewe ukasema ni Mungu. Hasa ukiwa huna neno la Mungu la kutosha na mafundisho sahihi ya kutosha ni rahisi kuingiziwa kitu tofauti na ukaona ni cha Kimungu.

Hakikisha unaweka bidii ya kusoma neno la Mungu, kuomba Mungu, kusoma vitabu vya watumishi wa Mungu vinavyohusu mahusiano, na kuhudhuria semina za mahusiano. Haya yote yanakusaidia kuwa na maarifa na uwezo wa kuweza kufanya maamzi sahihi pasipo kuwa na shaka yeyote.

Post a Comment

0 Comments