MHE. SAMIA ASIKILIZA KERO ZA WANANCHI KIGOMA.


Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mhe. Samia Suluhu Hassan amezungumza na Mwenyekiti wa shina (Balozi) Namba moja, katika Kata ya Kumunyika, Wilaya ya Kasulu, mkoani Kigoma Ndg. Juma Ahmed Rugina na kumpongeza kwa kuongoza shina hilo kwa miaka ishirini.

Balozi Mzee Rugina amezungumza na Mwenyekiti na Rais Mhe. Samia leo tarehe 19 Novemba, 2021 kupitia simu ya mkononi ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndg. Daniel Chongolo ambaye ametembelea shina hilo na kukagua uhai na uimara wa chama kwenye ngazi za mashina na kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo hayo.

Katika mazungumzo hayo, Balozi Rugina amempongeza Mwenyekiti na Rais Mhe. Samia kwa kuendelea kufungua fursa za maendeleo kwa wananchi wa Kasulu na mkoa wa Kigoma kwa ujenzi wa miundombinu ya barabara, afya na elimu ambapo amesema miaka ya nyuma wakati kama huu mifugo yao na vitu vingine vilikuwa vinauzwa kwa ajili ya michango ya kuchangia ujenzi wa madarasa, tofauti na mwaka huu ambapo fedha zote Mhe. Rais Samia amezitoa.

Aidha katika hatua nyingine, Balozi Rugina amemuomba Mwenyekiti na Rais Mhe. Samia kusaidia kutatua changamoto ya ukosefu wa karavati katika maeneo hayo, pamoja na  kadi za uanachama kwa wakereketwa wote wa CCM wa shina hilo pamoja na mashina mengine wilayani Kasulu na Mkoa wa Kigoma ambapo katika shina hilo kuna wanachama 64 na wakereketwa wengi wasio na kadi.

Kufuatia maombi hayo ya Balozi Rugina, Mwenyekiti Mhe. Samia amemuagiza Katibu Mkuu kushughulikia changamoto hiyo huku changamoto ya karavati akimuelekeza Mkuu wa Wilaya Kanali Isack Antony Mwakisu kushughulikia kwa haraka.

Wakati huo huo, Rais Samia amemuomba balozi huyo kuwahamasisha wanachama wake na wananchi kwa ujumla, kushiriki kwenye mambo ya maendeleo kikamilifu ikiwemo kuhakikisha wanachanjwa chanjo ya kujikinga dhidi ya Uviko 19.

Pamoja na kutembelea mashina, Katibu Mkuu ametembela na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani Kasulu ikiwemo mradi wa ujenzi wa Chuo cha Veta Kasulu, na ujenzi wa Shule ya Sekondari Mayonga.

Katibu Mkuu Ndg. Chongolo pamoja na Sekretarieti ya Halmashauri kuu ya CCM Taifa, wapo Kigoma kwa ziara ya siku mbili kwa lengo la kukagua utekelezaji wa ilani ya uchaguzi na kuhamasisha uhai wa mashina wa chama ngazi za Mashina.


Imetolewa na;

Said Said Nguya

Afisa Habari

Ofisi ya Katibu Mkuu

CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM).

Post a Comment

0 Comments