Mkuu wa Polisi Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma William Mwamafupa akizungumza juu ya umuhimu wa kutumia vema elimu ya usalama barabarani wakati akifunga mafunzo hayo kwa Wanafunzi wa shule za msingi na Sekondari ambayo yamefanyika katika shule ya msingi Likuyuseka.

Na.Amon Mtega,Namtumbo.

MKUU wa Polisi wa Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma William Mwamafupa  amewataka Wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari  pamoja na Raia wa kawaida wa  Wilayani humo  kuzingatia elimu ya usalama barabarani pindi wanapozitumia barabara hizo ili kuzuia ajali ambazo asilimia kubwa hutokana na uzembe wa utumiaji wa barabara ikiwemo na watumiaji wa vyombo vya moto.

Mwamafupa ambaye alikuwa mgeni rasmi ameyasema hayo wakati akifunga mafunzo ya usalama barabarani kwa wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari ,ambayo yamefadhiliwa na kampuni ya Mantra Tanzania Limited inayojishughulisha na madini ya Uranium yaliyopo katika mto Mkuju Wilaya ya Namtumbo mkoani humo .

Askari Polisi wa usalama barabarani Nurdin Ally Juma akiwafundisha Wanafunzi wa shule ya msingi ya Likuyuseka namna ya kuvuka barabara pindi wanapoenda shule na wanaporudi.

Mkuu huyo amesema kuwa kama jamii wakiwemo wanafunzi ikizingatia suala la usalama barabarani basi itasaidia kupunguza (Kuzuia) vitendo vya ajali barabarani ambazo zimekuwa zikigharimu maisha ya watu na kuzifanya baadhi ya familia kuwa masikini.

Hata hivyo mkuu huyo ameipongeza na kuishukuru kampuni ya Mantra kwa kutoa ufadhili wa mafunzo hayo ambapo hadi kuhitimisha shule 23 za Msingi na Sekondari zimepatiwa mafunzo ya usalama barabarani huku fedha Sh.Milioni 9.4 zilitolewa na kampuni hiyo kwaajili ya kuendesha mafunzo hayo.

Mkuu wa kitengo cha usalama barabarani Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma Evans Mayombe akiwataka wanafunzi na Wananchi kwa ujumla kuangalia sehemu sahihi za vivuko vya barabarani ili kuepusha ajali.

Naye mkuu wa kitengo cha usalama barabarani katika Wilaya ya Namtumbo Evans Myombe amesema kuwa baadhi ya wananchi wamekuwa wakipata ajali kwa uzembe wa kutokuchukua tahadhari ya kutokutambua sehemu sahihi ya waenda kwa miguu pamoja na  vyombo vya moto.

Pia askari Polisi anayesimamia dawati la Jinsia katika Wilaya hiyo Mwanaisha Monyo amesema kuwa licha ya suala la usalama barabarani lakini bado usalama hatarishi hasa kwa wanafunzi wa kike ambao baadhi yao hubakwa huku wazazi wao kuacha kutoa taarifa kwenye vyombo husika jambo ambalo linafanya vitendo hivyo vya kikatili viendelee kuwepo.

Askari Polisi wa dawati la Jinsia Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma Mwanaisha Monyo akiwataka Wazazi kuwalinda watoto wao kwa kutoa taarifa pindi watoto wao wanapofanyiwa vitendo viovu ikiwemo vya ubakwaji.

Mwanaisha amewaambia baadhi ya wazazi waliokuwa kwenye ufungaji wa mafunzo hayo kuwa wapeleke ujumbe kwa wenzao ambao hawakuwepo kwenye mafunzo hayo kuwa wawe na mazoea ya kuwakagua watoto wao hasa wakike ili kutambua kama wanafanya vitendo viovu.

Kwa upande wake meneja uhusiano wa kampuni ya Mantra Tanzania Limited Khadija Pallangyo amesema kuwa kampuni hiyo imefadhili mafunzo hayo baada ya kutambua baadhi ya Wananchi wakiwemo Wanafunzi wamekuwa hawafahamu suala zima la usalama barabarani.

Meneja Uhusiano wa Kampuni ya Mantra Tanzania Limited Khadija Pallangyo akizungumzia jinsi kampuni hiyo inavyofanya kazi na jamii

Meneja uhusiano huyo amesema kuwa licha ya kufadhili mafunzo hayo lakini bado kampuni hiyo imekuwa ikishirikiana na jamii katika utekelezaji wa miradi mbalimbali .