Mwenyekiti wa chama Cha Cha Mapinduzi CCM Mkoani Ruvuma Oddo Mwisho akizungumza kwenye hafla ya uwashaji wa umeme katika shule ya Sekondari ya Mkinga. |
Na Amon Mtega, Mbinga.
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi CCM Mkoani Ruvuma Oddo Mwisho ameupongeza Uongozi wa Shirika la umeme Tanzania (TANESCO) Mkoani humo kwa kutatua changamoto ya umeme katika shule ya Sekondari ya Mkinga inayomilikiwa na Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi .
Mwisho akizungumza kwenye hafla fupi ya uzinduzi wa uwashaji wa umeme huo katika Sekondari hiyo iliyopo Wilaya ya Mbinga Mkoani humo ambayo takribani miaka 40 tangu kuanzishwa kwake haikuwa na umeme amesema kuwa shirika la Tanesco Mkoani humo kupitia Meneja wake mhandisi Florence Mwakasege wameweza kuitatua changamoto ya ukosefu wa umeme katika Sekondari hiyo na kuwafanya wanafunzi wawe na uhakika wa kujisomea.
Mwenyekiti Mwisho ambaye amekuwa mgeni rasmi kwenye hafla hiyo ambayo imehudhuriwa na wadau na Viongozi mbalimbali akiwemo Mbunge wa Jimbo la Mbinga mjini Jonas Mbunda amesema kuwa Tanesco mkoa wa Ruvuma licha ya kupeleka umeme katika Sekondari hiyo lakini pia wamepeleka umeme katika Sekondari ya Namtumbo ambayo nayo inamilikiwa na Jumuiya hiyo.
Amesema kuwa kazi iliyofanywa na Shirika la umeme Mkoani Ruvuma kupitia Meneja wake mhandisi Florence Mwakasege ni kazi ambayo imekijengea heshima Chama Cha Mapinduzi na kuwa ndiyo utekelezaji wa Ilani ya chama hicho.
Hata hivyo mwenyekiti huyo ameipongeza Jumuiya ya Wazazi wa CCM Wilaya ya Mbinga pamoja na Uongozi wa shule hiyo kwa kazi nzuri ya kuimarisha miundombinu mbalimbali ikiwemo ya ujenzi wa jengo kubwa la utawala ambalo limefunguliwa na mwenyekiti huyo sambamba na kuzindua rasmi kidato cha tano na sita katika shule hiyo.
Licha ya pongezi hizo mwenyekiti huyo ameutaka Uongozi wa shule hiyo pamoja na Jumuiya hiyo kumtumia vema balozi wa shule hiyo Asha Chowo (Aisha) ambaye amekuwa akiitangaza shule hiyo katika maeneo mbalimbali na kuifanya shule hiyo iweze kuendelea kufahamika zaidi kwenye jamii.
Meneja wa Tanesco Mkoani Ruvuma mhandisi Florence Mwakasege akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa umeme huo katika shule ya Sekondari ya Mkinga. |
Kwa upande wake Meneja wa Tanesco mkoa wa Ruvuma mhandisi Florence Mwakasege wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi huo amesema kuwa shirika hilo limefanya kazi hiyo ili kutekeleza maagizo na jitihada za Serikali za kuboresha miundombinu mbalimbali kwa Wananchi pamoja na miundombinu ya shule ili kuwafanya wanafunzi waweze kuwa na mazingira bora ya kujisomea kwa kutumia mwanga wa umeme.
Hata hivyo Meneja huyo ameipongeza Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha miundombinu katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya Elimu na kuwafanya wanafunzi kuwa na ongezeko la ufaulu .
Naye mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM Wilaya ya Mbinga Erenest Mjirima ( Mgogo) amesema kuwa ofisi ya Wazazi Wilayani humo imekuwa na furaha kubwa kwa kuwa kulikuwa na kilio cha muda mrefu.
Pia Mbunge wa Jimbo la Mbinga mjini Jonas Mbunda wakati naye akitoa salamu kwa Wanafunzi hao amewataka wasome kwa bidii huku akiwaahidi ofisi yake itaendelea kushirikiana na Uongozi wa shule hiyo pamoja na Jumuiya ya Wazazi wa CCM katika kutatua changamoto zitakazojitokeza katika shule hiyo kwa kuwa ni moja ya historia kwake kutokana na kusoma shule hiyo.
Aidha katibu wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM Wilaya ya Mbinga Angelo Madundo kwenye hafla hiyo ametumia nafasi hiyo kutambua michango mbalimbali iliyotolewa na baadhi ya wadau kwa kuwapatia hati maalum za shukrani ( Vyeti ),ikiwemo Chama Cha waandishi wa Habari mkoa wa Ruvuma (Ruvuma Press Club).
Madundo amesema kuwa wadau hao wamekuwa wakijitoa kwa namna moja au nyingine na kuhakikisha mambo mbalimbali ya utekelezaji wa miundombinu katika shule hiyo yanasonga mbele .
Mkuu wa shule hiyo Jacob Msigwa akiwashukuru wadau mbalimbali ikiwemo TANESCO na Chama Cha Mapinduzi CCM pamoja na Jumuiya ya Wazazi amesema kuwa mafanikio hayo yanafikiwa baada ya kushirikiana kikamilifu katika nyanja zote hivyo ameendelea kuomba ushirikiano huo ili kuifanya shule hiyo kuwa mfano bora mbele za jamii na kuwa wamejipanga vema kuongeza ufaulu zaidi.
0 Comments