Na Amon Mtega,Mbinga.
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi CCM Mkoani Ruvuma Oddo Mwisho ameipongeza Jumuiya ya Wazazi wa CCM Wilaya ya Mbinga kwa kubuni Bonanza ambalo limeenda sambamba na ufanyaji usafi kwenye maeneo muhimu ya Jamii.
Mwisho ambaye amekuwa mgeni rasmi kwenye bonaza hilo amezitoa pongezi hizo wakati akizungumza na washiriki mbalimbali wa mbio hizo kutoka kwenye taasisi za Serikali na taasisi za watu binafsi akiwemo na Mbunge wa Jimbo la Mbinga mjini Jonas Mbunda ambaye ameshiriki kufanya usafi kwa mikono yake kwenye baadhi ya maeneo ya kijamii ambayo ni kwenye Soko kuu la Mbinga,Hospitali ya Halmashauri ya Mbinga mji(Mbuyula) na Kituo cha mabasi Cha Mbinga (Stendi) mwenyekiti huyo amesema Jumuiya ya Wazazi wa CCM Mbinga wanatakiwa kuigwa ubunifu huo na Jumuiya zingine.
Amesema kuwa kumekuwepo na baadhi ya Jumuiya kujisahau kuwa matukio kama hayo ya kijamii yanatakiwa kufanywa na Chama Cha Mapinduzi CCM pekee jambo ambalo amesema siyo kweli bali hata Jumuiya zingine zinaweza zikafanya kazi za kijamii kama ilivyofanya Jumuiya ya Wazazi wa CCM Wilaya ya Mbinga.
"Mimi nawapongezeni sana Jumuiya ya Wazazi wa CCM Wilaya ya Mbinga akiwemo mwenyekiti Erenest Mjirima (Mgogo) pamoja na katibu wa Jumuiya hiyo Angelo Madundo kwa kushirikiana na Sekeletarieti yenu na kulibuni jambo hili nawapongezeni sana"amesema Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho.
Aidha katika hatua nyingine mwenyekiti huyo akiwa katika Hospitali ya Halmashauri ya mji wa Mbinga (Mbuyula)ametoa pole kwa wagonjwa pamoja na kutoa miche ya sabuni kwa Wakinamama ngojea na waliojifungua huku akiwataka waendelee kuiamini Serikali yao ya awamu ya sita inayoongonzwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa inaendelea kuboresha miundombinu mbalimbali ikiwemo maeneo ya Afya.
Mbunge wa Jimbo la Mbinga mjini akipanda mti katika eneo la Hospitali ya Mbinga -Mbuyula ikiwemo ni sehemu ya kuihamasisha jamii namna ya utunzaji wa mazingira. |
Kwa upande wake mbunge wa Jimbo la Mbinga mjini Jonas Mbunda amesema kuwa ataendelea kushirikiana na Wananchi wake wa Jimbo hilo kutatua changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa kero kwa jamii huku akiwataka waendelee kuiunga mkono Serikali yao ya awamu ya sita kwa uchapaji kazi wake.
Hata hivyo mbunge huyo ambaye ameshiriki matukio yote kwenye bonanza hilo pia ametoa zawadi ya jezi na mpira kwa shule ya Sekondari ya Mkinga Wilaya ya Mbinga inayomilikiwa na Jumuiya ya Wazazi wa CCM ambao pia walishiliki zoezi hilo kikamilifu.
Naye mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM Wilaya ya Mbinga Erenest Mjirima (Mgogo)akizishukuru taasisi zilizoweza kushiriki zoezi hilo ikiwemo ofisi ya mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbinga mji ambayo mkurugenzi wake Grace Quintine pamoja na taasisi za watu binafsi ikiwemo Kampuni ya Ovans Construction Ltd, amesema kuwa zoezi hilo litakuwa linafanyika kila baada ya miezi mitatu.
Aidha akitolea ufafanuzi juu ya bonanza hilo katibu wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM Wilaya ya Mbinga Angelo Madundo amesema kuwa Jumuiya imebuni zoezi hilo baada ya kutambua kuwa kumekuwepo na baadhi ya wanajamii kujisahau katika maeneo yao wanayoyafanyia kazi hasa kwenye vituo vya mabasi (Stendi)na Sokoni kutokuwajibika na usafi jambo ambalo Jumuiya hiyo inapita kuwakumbusha umuhimu wa kufanya usafi ambao utawasaidia kulinda Afya zao.
Hata hivyo Jumuiya hiyo licha ya kufanya zoezi la usafi katika maeneo hayo lakini bado imeshiriki kupanda miti katika eneo la Hospitali ya Halmashauri hiyo ambapo zoezi hilo limeongozwa na mwenyekiti Oddo Mwisho pamoja mbunge Jonas Mbunda ikiwa ni sehemu kuwahimiza Wananchi kutunza mazingira.
0 Comments