RUVUMA:WAKANDARASI WA UMEME WATAKIWA KUTUMIA MAFUNDI UMEME WENYE LESENI ZA EWURA.


Mkuu wa Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma Pololet Mgema akizungumza na mafundi umeme juu ya umuhimu wa kuwa na Leseni kutoka Ewura.


Na.Amon Mtega,Ruvuma

MKUU wa Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma Pololet Mgema amewataka wakandarasi wa umeme wa Mkoani humo kuwatumia mafundi ambao wamehitimu vyuo vinavyotambulika pamoja na wenye Leseni za Ewura ili kuepusha changamoto mbalimbali zilizokuwa zikijitokeza kwenye kazi hiyo.

Wito huo ameutoa wakati akifungua mafunzo kwa mafundi umeme wa mkoa huo yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA)ambayo yamehusu  kanuni za ufungaji wa umeme kwenye Nyumba za watu pamoja na Nyumba za umma.
Mgema ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye ufunguaji wa mafunzo hayo amesema kuwa kama wakandarasi wa umeme watafanya kazi ya kuwatumia mafundi wa umeme waliohitimu kwenye vyuo vinavyotambuliwa itasaidia kupunguza changamoto za mafundi hao kuendelea kuitwa vishoka.

Aidha katika hatua nyingine mkuu huyo ameipongeza Ewura kwa kutoa mafunzo hayo kwa mafundi umeme wa mkoa huo kwa kuwa sekta ya umeme ndani ya mkoa huo inapanuka hadi vijijini hivyo itawasaidia mafundi hao kuwa na uwigo mpana wa kufanyia kazi .
Kaimu mkurugenzi wa Ewura ambaye pia ni Meneja mawasiliano Ewura, Titus Kaguo akizungumzia utendaji kazi wa Ewura kwa mafundi umeme wa mkoa wa Ruvuma wakati wakipatiwa mafunzo.

Kwa upande wake kaimu mkurugenzi wa Ewura, Titus Kaguo akitoa taarifa ya ufanyaji kazi wa mamlaka hiyo amesema  wametoa mafunzo hayo kwa makundi mawili la Wafanyakazi wa Tanesco pamoja na mafundi wa umeme baada ya kubaini kuwepo kwa mafundi wasiokuwa na Leseni zinazotambuliwa ikiwemo ya Ewura.

Kaguo ambaye pia ni meneja mawasiliano Ewura akizungumzia kuhusu utendaji kazi wa mamlaka hiyo amesema kuwa katika kipindi cha miaka 15 Ewura imeweza kujiimarisha na kupanua wigo wake kwa kusogeza huduma zake karibu na wananchi pamoja na kutatua changamoto mbalimbali kutokana na huduma zinazodhibitiwa na Mamlaka ambapo awali huduma hizo zilikua zikipatikana Dar-es Salaam pekee.
Mmoja wa mafundi umeme Wilon Kapinga Mkoani Ruvuma akizungumzia mafanikio ya mafunzo hayo.

Naye mmoja wa mafundi hao Wilon Kapinga amesema kuwa mafunzo hayo yatawasaidia kuondokana na changamoto mbalimbali zilizokuwa zikijitokeza kabla ya kupatiwa mafunzo hayo.

Hata hivyo Ewura imegawa Leseni kwa baadhi ya mafundi hao ambao walifikisha vigezo vinavyotakiwa huku ambao hawakutimiza vigezo wametakiwa wavitimize ili wapatiwe Leseni.

Post a Comment

0 Comments