NA AMON MTEGA, MBINGA.
WABUNGE wa Viti maalum wa Mkoa wa Ruvuma Jacqueline Ngonyani (Msongozi) na Mariam Nyoka kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi CCM wameunga mkono jitihada zinazofanywa na Jumuiya ya Wanawake wa CCM (UWT) Wilaya ya Mbinga Mkoani humo za ujenzi wa Ukumbi pamoja na ujenzi wa Nyumba ya Katibu wa Jumuiya hiyo.
Wameunga mkono wabunge hao kwa kuchangia ujenzi wa miradi hiyo wakati wa kikao cha baraza la wanawake wa CCM ngazi ya Wilaya ambalo lilienda sambamba na harambee ya kuchangia ujenzi wa miradi hiyo.
Mwakilishi wa mkuu wa Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma Ahsante Luambano akiwasilisha mchango uliotolewa na mkuu wa Wilaya hiyo Aziza Mangosongo wakati kikao cha baraza la UWT Wilaya ya Mbinga |
Wakichangia kwenye harambee hiyo Mbunge Jacqueline Ngonyani (Msongozi) ametoa ahadi ya kuchangia Sh.Milioni tano (sh,5,000,000=) huku Mbunge Mariam Nyoka amechangia bati sabini (70)na fedha Sh.Milioni moja na laki nne (Sh.1,400,000=)ambazo ziliwasilishwa na katibu wake Thabita Lungu.
Akizungumza Mbunge Jacqueline Ngonyani kwenye baraza hilo ambalo wadau mbalimbali walialikwa ameipongeza Jumuiya hiyo kwa kuibua miradi ambayo itaifanya Jumuiya hiyo kuendelea kusimama imara katika suala zima la kiuchumi.
Wajumbe wa Jumuiya ya Wanawake wa CCM (UWT)Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma wakiwa wameshika mbegu za Alizeti walizogawiwa na Mbunge wa Viti maalum Jacqueline Ngonyani (Msongozi). |
Mbunge Ngonyani sambamba na kuchangia fedha hizo lakini aligawa mbegu za Alizeti kwa wajumbe 147 zenye ujazo wa kilo mbili ambazo hutosheleza kila mjumbe kuwa na eka moja ya shamba la Alizeti.
Ugawaji wa mbegu hizo bure kufuatia ahadi ambayo aliiahidi kwa wajumbe hao na kuwa atapita kugawa kwa wajumbe wote wa mkoa wa Ruvuma mbegu hizo kwa lengo la kumtaka mwanamke ajikwamue .
Kwa upande wake Tabitha Lungu ambaye ni katibu wa mbunge Mariam Nyoka wakati akitoa mchango wa bati na fedha hizo amesema kuwa mbunge huyo amemtuma achangie harambee hiyo kutokana nayeye kuwa udhuru na kuwa ataendelea kuunga mkono jitihada zinazofanywa na jumuiya hiyo,huku katibu huyo naye amechangia mifuko mitano ya saruji nje ya mchango wa mbunge huyo.
Licha ya wabunge hao kuchangia lakini kumekuwepo na wachangiaji wengine akiwemo mkuu wa Wilaya ya Mbinga ambaye aliwakilishwa na Ahsante Luambano ambaye alitoa sh.200,000=pamoja na mifuko 15 ya Saruji ambayo itatolewa na mwakilishi huyo ,huku madiwani wa viti maalum nao wamechangia fedha kwa viwango mbalimbali.
Katibu wa CCM wa Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma Jacob Siay ameipongeza UWT Wilaya ya Mbinga kwa kuendelea kuwa wamoja kuijenga Jumuiya hiyo. |
Aidha katibu wa CCM Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma Jacob Siay ameipongeza Jumuiya hiyo kwa kuwa na mshikamano huku akiwataka waendelee kuwa na mshikamano huo ili kukifnya Chama cha Mapinduzi CCM kuwa na nguvu ya kuendelea kushika dola.
Siay ambaye ni katibu mpya kwenye Wilaya hiyo amesema kuwa wanawake wana kila sababu ya kujivunia maendeleo yanayofanywa na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan na kuziunga mkono kazi hizo.
Naye katibu wa Jumuiya ya UWT CCM Wilaya ya Mbinga Martina Katyale awali akisoma taarifa ya utekelezaji wa Jumuiya hiyo amesema kuwa mpango wa kujenga ukumbi na Nyumba ya katibu uliibuliwa na wajumbe wajumuiya hiyo wakiwemo madiwani wa viti maalumu.
Hata hivyo katibu Katyale amewashukuru Wabunge wote wa majimbo ya Mbinga pamoja na wabunge wa Viti maalum pamoja na wadau mbalimbali wakiwemo madiwani kwa michango yao kwenye Jumuiya hiyo.
0 Comments