WAKAZI wa Mkoa wa Ruvuma wametakiwa kutumia wiki ya sheria kwenda kupata elimu juu ya madai mbalimbali ambayo wamekuwa wakikuta nayo kwenye jamii ili waweze kujenga uelewa pindi wanapokutana na madai hayo.
Wito huo umetolewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama kuu Kanda ya Songea Sekela Moshi wakati akitoa hotuba ya uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya utoaji elimu ya sheria inayofanyika katika viwanja vya soko kuu la Songea mjini ambayo yameanza Januari 23 mwaka huu na kilele Mosi Februari yameenda sambamba na kauli mbiu ya Zama za mapinduzi ya nne ya Viwanda ,Safari ya maboresho kuelekea mahakama mtandao.
Jaji Moshi akitoa hotuba hiyo mbele ya mgeni rasmi Dkt Julius Ningu mkuu wa Wilaya ya Namtumbo ambaye amemuwakilisha mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Balozi Wilbert Ibuge amesema kuwa ni ukweli usiopingika Wananchi wengi wamekuwa hawazitambui kazi zinazofanywa na mahakama pindi wanapohitaji msaada wa kisheria ,hivyo wanatakiwa kutumia wiki hiyo kikamilifu kwa kujipatia elimu.
Amesema kuwa mahakama zimejipanga vema kuendelea kuboresha namna ya usikilizaji wa madai kwa kutumia mifumo mbalimbali ikiwemo ya kisasa (TEHAMA) ambayo itawafanya wananchi wazidi kuwa na uelewa pindi wanapotumia mitandao ya kiteknolojia namna ya kupata haki za madai yao .
Mosha amesema kuwa katika wiki ya sheria Mahakama imewahusisha wadau mbalimbali katika mfumo wa utoaji wa haki kama vile ofisi ya mwanasheria mkuu wa Serikali ,Ofisi ya mkurugenzi wa mashitaka ,Ofisi ya wakili mkuu wa Serikali ,Tume ya haki za Binadamu na Utawala bora,Taasisi zinazotoa msaada wa kisheria (Legal Aid) Magereza,Takukuru na Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) ambazo hujumuika pamoja kutoa elimu na ushauri wa kisheria kwa wananchi bila malipo.
Kwa upande wake katibu wa Chama cha mawakili Tanganyika (TLS) mkoa wa Ruvuma Naomi John amesema kuwa Chama hicho kimekuwa kikitoa ushauri wa kisheria kwa wale wasio na uwezo baada ya kuwafanyia tathmini pamoja na kutoa elimu kupitia vyombo vya habari mbalimbali ikiwemo redio .
Naye Wakili wa Serikali katika taasisi ya Mamlaka ya Maji Safi na usafi wa Mazingira Songea Abely Ngilangwa amesema kuwa kazi kubwa ya wakili wa Serikali ni kuishauri Serikali pale panapokuwa na mashauri yanayoihusu Serikali ili kuifanya iwe kwenye msimamo sahihi isiweze kuingia kwenye migogoro ambayo inaweza kuepukika .
Ngilangwa amesema kuwa hakuna mashauri (Kesi)ambazo mawakili wa Serikali wakasema wameshindwa bali ni namna ya kujipanga jinsi ya kuweza kuishauri Serikali kwa kuwa mashauri yanakuwa na mambo mengi ambayo yanatakiwa kuwa na umakini.
Kwa upande wake mgeni rasmi Dkt Julius Ningu ameipongeza Mahakama jinsi wanavyoendelea kuboresha namna ya utoaji huduma kwa Wananchi jambo ambalo litawasaidia wananchi kupatiwa huduma kwa wakati.
Dkt Ningu ambaye amemuwakilisha mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Bregedia Jenerali Balozi Wilbert Ibuge amesema kuwa Mahakana zimepunguza malalamiko mengi kwa Wananchi na kufanya waendelee kuwa na imani na mahakama zao.
Aidha katika hatua nyingine Dkt Ningu ameipongeza mahakama ya mkoa wa Ruvuma kwa ujenzi wa vituo vya jumuishi vya utoaji haki na ukarabati wa majengo yake ili kuendana na mapinduzi ya nne ya viwanda ,matumizi ya tehema katika shughuli zake zote za utoaji haki,usikilizwaji wa mashauri kwa njia ya video.
0 Comments