JESHI la Polisi Mkoani Mbeya linamshikilia mwanafunzi wa kidato cha tano katika Shule ya Sekondari Iduda aitwaye Humphrey Ngogo (17)kwa tuhuma za mauaji ya mwanafunzi mwenzake Faraja Kasole (16)wa kidato cha nne shule ya sekondari Sinde.
Mtuhumiwa alichukua uamuzi wa kumpiga na shoka marehemu baada ya kuzidiwa nguvu wakati akijaribu kumbaka.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Kamanda wa Polisi wa Mbeya, Ulrich Matei alisema kuwa tukio hilo limetokea Septemba 2 mwaka huu majira ya saa 10.45 jioni katika mtaa wa Mkuyu kata ya Iganzo Mkoani Mbeya.
Matei alisema kuwa chanzo cha tukio hilo ni tamaa za kimwili ambapo Mtuhumiwa alijaribu kumbaka marehemu lakini baada ya kuzidiwa nguvu ndipo Mtuhumiwa alipochukua shoka na kumpiga nalo kichwani marehemu.
Aidha Kamanda Matei alisema kuwa kabla ya tukio hilo, mtuhumiwa alifika nyumbani kwa marehemu ambaye kwa muda huo alikuwa peke yake na kisha kumvamia chumbani kwake kwa nia ya kumbaka na alipozidiwa nguvu ndipo aliamua kuchukua shoka na kumpiga nalo
Hata hivyo Matei alisema baada ya tukio hilo Mtuhumiwa alikamatwa na Polisi na upelelezi wa shauri hilo unaendelea na mara baada ya kukamilika atafikishwa mahakamani.
Aidha Kamanda huyo alisema jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linalaani tukio hilo baya kutokea na linatoa pole kwa wazazi na familia ya marehemu.
Hata hivyo Matei alitoa rai kwa wazazi na walezi kujenga tabia ya kuzungumza na watoto wao na kuwataka kujikita zaidi kwenye masomo na kuachana na tamaa za kimapenzi wangali masomoni ili kuepuka matukio kama haya.
0 Comments