MAHAKAMA ya hakimu mkazi wilaya ya Bukoba mkoani Kagera imewahukumu mchungaji Merchades Mugishagwe kutumikia kifungo cha miezi 18 gerezani na kulipa faini shilingi milioni tatu, na mke wake Agripina Maganja kifungo cha nje miezi sita, baada ya kuwatia hatiani kwa makosa matatu.

Makosa hayo ni kushindwa kutekeleza wajibu wake kama mzazi, kushindwa kupeleka watoto shule na kujihusisha na vikundi visivyotakiwa kijamii.

Hukumu hiyo imetolewa na hakimu mfawidhi wa mahakama hiyo Daniel Nyamkerya baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka.

Kufuatia hukumu hiyo  mke wa mchungaji huyo Agripina Maganja ambaye amehukumiwa kifungo cha nje, amepewa masharti ya kutotenda kosa lolote katika kipindi hicho cha miezi sita.

Wakili wa serikali Grey Uhagile amesema kuwa katika hukumu hiyo mchungaji huyo amehukumiwa adhabu ya miezi sita kwa kila kosa na kwa kuwa atatumikia adhabu hiyo kwa wakati mmoja, atakaa gerezani kwa muda wa miezi sita.

Amesema mchungaji na mke wake walikuwa na mashtaka manane, na wametiwa hatiani kwa  makosa matatu ya mwanzo ambayo ni kushindwa kutekeleza majukumu yao kama wazazi chini ya sheria ya mtoto ya mwaka 2009, kushindwa kuwapeleka watoto shuleni wenye umri wa kwenda shule kinyume na utaratibu, na pia walishtakiwa chini ya sheria ya jamii kwa kujihusisha na vikundi ambavyo havitakiwi kijamii.

Ushahidi katika kesi hiyo ambayo ilisimamiwa na wakili wa utetezi Rogate Assey ilifungwa Agosti 12 mwaka huu kwa kusikiliza mashahidi wawili kati ya watatu, baada ya shahidi namba tatu aliyetajwa na washtakiwa hao kuwa ni Mungu kushindwa kufika mahakamani.

 

Mchungaji Merchades Buberwa Mugishagwe na mke wake Agripina Maganja walifikishwa katika mahakama hiyo Februari mwaka huu wakikabiliwa na mashtaka manane ambayo ni kushindwa kutimiza wajibu wao kama wazazi wa kuwapeleka watoto wao watatu shule, wakidai kufanya hivyo ni dhambi, maana maandiko ya Mungu hayaruhusu watoto kwenda shule.