MMOJA AFARIKI KUFUATIA VURUGU ZA WAFUGAJI NA POLISI


 Akizungumzia tukio hilo kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma Joseph Konyo amesema tukio hilo  limetokea Agosti mosi  mwaka huu majira ya saa mbili asubuhi katika eneo la Nakayombo mashambani wakati Jeshi la Polisi Wilayani humo lilipokuwa limeenda kuwakamata watuhumiwa ambao ni wafugaji kwa kosa la kulishia mifugo yao kwenye mazao ya wakulima wa Wilaya hiyo.

 Kamanda Konyo amesema Polisi walipofika katika eneo la tukio inadaiwa kuwa wafugaji hao nao walijikusanya huku wakiwa na silaha za kijadi za aina mbalimbali ikiwemo mikuki  na kuanza kufanya vurugu licha ya Askari Polisi kutumia mabomu ya machozi lakini hawakutii sheria bila shuruti jambo lililopelekea mfugaji Julius Mangule ambaye hakuwa moja ya watuhumiwa kufariki Dunia kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali.

Kwa mujibu wa kamanda Konyo amesema mara kadhaa wafugaji hao wamekuwa wakiwafanyia vurugu wakulima wa Wilaya hiyo kwa kulishia mifugo yao kwenye mazao ya yao jambo ambalo limekuwa likihatarisha Amani baina ya pandehizo mbili na kuwafanya waishi kwa uhasama.

Akitolea mfano kwa baadhi ya matukio baina ya wakulima na wafugaji amesema mnamo Julai 23 mwaka huu katika mashamba yaliyopo katika Kijiji cha Mchomoro Wilaya ya Namtumbo mkazi mmoja Zuberi Hassan (52)wakati akilinda mazao yake yasilishiwe na mifugo ghafla lilimjia kundi la wafugaji kisha kumtishia na silaha za kijadi ikiwemo mikuki jambo ambalo lilimfanya mkulima huyo kukimbia na kuacha mazao yake yakiliwa na mifugo yao

 Akilitaja tukio lingine kuwa katika Kijiji hichohicho cha Mchomoro Wilaya ya Namtumbo Athumani Salumu(32)mnamo Agosti mbili mwaka huu akiwa kwenye shamba lake la mpunga  alivamiwa na kundi la wafugaji wakiwa na mifugo,inadaiwa kuwa walimjeruhi kichwani na kisha mkulima huyo aliokolewa na wasamaria wema ambao walimkimbiza Hospitalini kwa matibabu.

 Kufuatia matukio hayo kamanda wa Polisi wa mkoa huo ametoa rai  kwa makundi yote mawili kutii sheria bila shuruti na kuacha tabia ya kulizuia Jeshi la Polisi linapofanya kazi ya kulinda raia na mali zao pamoja na kuwakamata wahalifu ambao wamekuwa wakiikosesha jamii kuishi kwa Amani.

Post a Comment

0 Comments