MGANGA Mkuu wa Serikali, Dkt. Aifello Wedson Sichalwe leo agosti 13 ametoa ufafanuzi juu ya 'clip' inayosambazwa mitandaoni ikimuonesha Dkt. Bulugu wakati wa kuongea mada yake alivyopatwa na hali ya kizunguzungu hali iliyotafsiriwa tofauti na wapotoshaji.
Katika taarifa yake hiyo Dkt. Sichwale ameeleza:"Mnamo tarehe 12/08/2021 kulikuwa na mdahalo wa wanasayansi kujadili masuala mbalimbali ya UVIKO-19 na kutoa elimu kwa wananchi waliokuwa wanafuatilia mdahalo huo, Mgeni rasmi alikuwa Dkt. Dorothy Gwajima (Mb), Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto
"Wakati Dkt. Sospeter Bulugu akiongea mada yake alipatwa na hali ya kizunguzungu hivyo, wataalamu kulazimika kumpatia huduma ya kwanza na Uchunguzi ulionesha kuwa hali hiyo ilitokana na kushuka kwa sukari kwenye damu ambayo kitaalamu inajulikana kama Hypoglycemia.
"Kwenye video fupi inayozunguka kwenye mitandao ya kijamii ikionesha tukio hilo imesikika sauti ya Waziri wa Afya Dkt Dorothy Gwajima ikihoji iwapo Dkt. Bulugu alikuwa amepata chanjo? Baada ya kuthibitika kuwa hajawahi kupata chanjo ya UVIKO-19 sauti ya Mheshimiwa Waziri wa Afya ilisikika tena ikisema, basi amepatwa na kushuka kwa sukari hasa ukizingatia tangu kuanza kwa mkutano huo hakukuwa na mapumziko ya chai ambapo alielekeza apewe huduma ya kwanza ikiwemo kinywaji chenye sukari na pipi ambapo, baada ya hapo hali yake ilitengemaa''.
"Wakati huohuo ilibainika kuwa vyombo vya habari vilikuwa vikichukua tukio hilo jambo ambalo ni kinyume na maadili ya kitabibu pale mteja anapokuwa anapatiwa huduma kwenye mikono ya kitaalam huku akiwa hajaridhia huduma hiyo iwe wazi.
"Hivyo, kwa kutumia kiapo na maadili ya taaluma yake kama daktari Mheshimiwa Waziri wa Afya, Dkt. Dorothy Gwajima, aliwataka wanahabari wasichukue tukio hilo. Hata hivyo, imebainika kuwa wapo waliochukua na kuzisambaza na matokeo yake zimetumika kupotosha vikihusisha tukio hilo na madhara ya chanjo, jambo ambalo siyo kweli.
Hivyo, niwaombe watu wote watakaofanikiwa kukutana na taarifa za kuwa Dkt. Sospeter Bulugu alipata madhara ya chanjo wazipuuze kwani ni uzushi kama uzushi mwingine wowote.
"Aidha, wapuuze madai kuwa Waziri wa Afya, alitaka kuficha jambo kuhusu madhara ya chanjo kwani kuvitaka vyombo vya habari visichukue tukio hilo Waziri wa Afya alikuwa anatekeleza majukumu yake ya maadili ya kitaaluma pale panapokuwa na mteja anayepokea huduma za afya ambaye hajaridhia kwa hiari yake kwamba huduma hiyo iwe wazi (informed consent).
"Wizara haijapendezwa na jinsi ambavyo taarifa hizo zimechukuliwa bila ridhaa ya mteja na zilivyotumika kupotosha kwa nia ya kupaka matope au dosari zoezi la chanjo ya UVIKO-19 linaloendelea nchini.
"Napenda kuwahakikishia wananchi wote kuwa, zoezi la chanjo hiyo linaendelea vizuri, niwaombe wote wenye mahitaji wa huduma hii wajitokeze kupokea.
"Wizara itaendelea kutoa elimu ya afya na ufafanuzi muda wote". Ilieleza taarifa hiyo ya Mganga mkuu wa Serikali.
0 Comments