KUTOKANA na janga la Corona kuendelea kutikisa maeneo mbali mbali ya nchi na dunia ,mkuu wa mkoa wa Iringa Queen Sendiga amelazimika kuwatimua waombolezaji ambao walikuwa wamefurika katika chumba cha kuhifadhia maiti Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Iringa kwa ajili ya kufuata miili ya ndugu zao .
Mkuu huyo wa mkoa alifika eneo hilo la chumba cha kuhifadhia maiti baada ya uongozi wa Hospitali hiyo kueleza kero ya wananchi kusongamana katika eneo hilo kinyume na maelekezo ya wizara ya afya .
Akielezea sababu ya kuwafukuza waombolezaji hao amesema hali ya janga la UVIKO-19 ndani ya mkoa wa Iringa ni kubwa na hivyo lazima kila mwananchi kuchukua tahadhari kwa kuzingatia maagizo ya wizara ya afya na moja ya maagizo hayo ni misongamano isiyo ya lazima .
" Naomba kuagiza kuanzia leo hii watakaoruhusiwa kufika chumba cha kuhifadhia maiti kuchukua mwili ni watu wanne pekee na sio zaidi ya hapo walinzi hakikisheni hapa nje hakuna msongamano wowote wakati wote hebu tazama hapa leo zaidi ya watu 100 wamekaa nje ya chumba cha kuhifadhia maiti na hao wamefuata mwili mmoja tu na jiulize hawa wote wamekuja kubeba mwili huu mmoja hapana haiwezekani kuacha misongamano kama hii" alisema huku akiwataka wafiwa hao kuanza kutawanyika eneo hilo.
Pia ameagiza ofisi ya mkurugenzi wa Halmashauri ya manispaa ya Iringa kutumia vyombo vya habari kutangazia wananchi juu ya kuepuka mikusanyiko katika eneo hilo na maeneo mengine na akaagiza wale wanaokwenda kuona wagonjwa wasizidi zaidi ya wawili kwa mgonjwa mmoja .
Mganga mfawidhi wa hospitali ya rufaa ya mkoani Iringa Dkt Alfredy Mwakalebela amesema kumekuwepo na changamoto kubwa sana katika eneo hilo la chumba cha kuhifadhia maiti kwa wananchi kulazimisha kuingia getini kusubiri miili ya jamaa zao .
Kwa upande wake kamanda wa Polisi wa mkoa wa Iringa Juma Bwire ameagiza mmiliki wa kampuni inayohusika na ulinzi katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Iringa kufika ofisini kwake ili kupewa maelekezo ya nini cha kufanya kwa ajili ya kuthibiti misongamano katika eneo hilo la Hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa .
0 Comments