Mila na desturi zilizopitwa na wakati kwenye jamii zimetakiwa kuachwa kutumiwa na jamii ya sasa kwani zimetajwa kuchangia kwa namna moja ama nyingine kuongezeka kwa matukio ya ukatili wa kijinsia kwenye jamii.
Katika kuhakikisha mila hizo hazitumiki tena au zinaboreshwa wadau mbalimbali wa maendeleo ya jamii wamekuwa wakijitokeza kutoa elimu mahususi ili kujenga uelewa wa madhara yake kwa faida ya vizazi vilivyopo na vijavyo.
Agnatha Rutazaa ni mkurugenzi mtendaji wa shirika lisilo la kiserikali la TUSONGE-CDO linalojihusisha na haki za binadamu,pamoja na kujenga uelewa na utetezi usawa kwenye jamii liliopo wilayani hapa ambapo amesema bado uelewa wa haki katika jamii umeghubikwa na mila zilizopitwa na wakati.
Rutazaa amesema jamii zilizopo mkoani Kilimanjaro zimekuwa zikitumia vibaya matumizi ya jani la 'sale' ambalo hutumiwa mara kadhaa na kabila la wachaga katika kutafuta suluhu au amani pale inapoonekana kupotea
"Jani la 'sale'ni amani na upendo hata ukimkosea mtu unaenda kuomba msamaha ukiwa nalo mkononi na ilivyoaminika mtu akikuomba msamaha akiwa nalo usipomsamehe utajipatia laana na mikosi".
Kutokana na imani ya matumizi ya jani hilo wapo ambao kwenye jamii hufanyiwa ukatili na badala ya kwenda katika vyombo vya sheria anaombwa kupitia jani hilo hivyo haendi au haonyeshi ushirikiano kwa vyombo husika.
"Unakuta mtu kafanyiwa ukatili labda na mjomba wake au baba na akihojiwa polisi anazungumza vizuri tu ila kesi ikienda mahakamani ghafla mtu anageuka bubu hapo ujue tayari ameshaenda kuombwa na sale" Rutazaa.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo lengo la matumizi ya jani hilo ilikuwa ni kuomba amani na maridhiano katika jamii hususani kwa kabila la wachaga lakini sasa hali imebadilika na kuwa watu wanatumia kimvuli katika kuhalalalisha ukatili wa kijinsia.
"Nadhani mila na desturi za watu ziendelee kama ambavyo zilivyozoeleka lakini pia watu wasijifiche nyuma ya hili 'sale' katika kuendeleza vitendo vya kikatili hususani kwa mabinti na wazee ambao wanaonekana kuwa ni wahanga wakubwa" Rutazaa
Nae Wakili Virginia Silayo ambaye ni mkurugenzi wa shirika la lisilo la kiserikali lijulikanalo kama AJISO linalofanya kazi zake katika wilaya ya Rombo,Same,Mwanga na Dodoma amesema jani hilo lilikuwa na maana lakini kwa sasa ni kama linatumiwa vibaya.
"Jani hili lilikuwa na maana nzuri lakini kwa siku za karibuni ni kama limebadilishwa matumizi na matokeo ndio kuongezeka kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia kwenye jamii hususani maeneo ya Vijijini".
0 Comments