Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Tanzania DCI Camilius Wambura amesema  Hamza Mohamed alikuwa gaidi na tukio alilofanya ni la kujitoa muhanga.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari, DCI Wambura amesema kuwa mara baada ya tukio hilo walianza uchunguzi na kutaka kujua kwanini alifanya tukio hilo, yeye ni nani na nani mshiriki mwenzake wa tukio hilo.

‘’Hamza Mohamed ni mtu alikuwa akiishi kisiri na amegubikwa na viashiria vyote vya kigaidi, amekua akijifunza mambo ya kigaidi kupitia mtandao’. Anasema DCI Wambura.

Ameongeza pia uchunguzi wao umebaini kuwa Hamza alikuwa gaidi wa kujitoa muhanga.

DCI Wambura ameongeza Hamza alikuwa akifanya ugaidi kupitia mtandao kwa kujifunza na kuwa na mawasiliano na makundi kama Al-shabab na ISIS.

Aidha madai ya kuwa Hamza alikuwa na madini kama ambavyo taarifa hizo zilivyosambaa kwenye mitandao ya kijamii, Wambura amesema hakuwa na madini yoyote na uchunguzi umebaini shughuli za mgodi wao zilisimama kwa muda mrefu sasa.

Katika shambulio hilo lililotokea wiki iliyopita Hamza Mohamed alifanya mashambulizi na kuua watu wanne-Polisi watatu mlinzi mmoja wa kampuni binafsi kisha baadaye na yeye kuuawa na polisi.