Mahakama ya juu nchini Marekani imekataa shauri la kuzuia sheria mpya iliyopitishwa katika jimbo la Texas lililo kusini mwa nchi hiyo, ambayo inapiga marufuku utoaji mimba pale mapigo ya moyo wa mtoto aliyemo tumboni yanapoweza kusikika kwa kutumia vifaa vya tiba. 

Watetezi wa haki ya kutoa mimba wanasema mapigo hayo yanaweza kusikika baada ya wiki sita za kupata mimba, na wanasema wakati huo wanawake wengi wanakuwa hawana habari kuwa ni wajawazito. 

Sheria hiyo iliyosainiwa jana na Gavana wa Texas Greg Abbot inalinda mimba zote, hata zilizotokana na ubakaji.

Uamuzi wa mahakama ya juu yenye majaji tisa, ambao ni ushindi kwa wapinzani wa uavyaji wa mimba, ulipitishwa na majaji watano, watatu miongoni mwao wakiwa wateule wa rais wa zamani Donald Trump.

 Rais Biden amesema ataendelea kupigania haki ya kutoa mimba.