Kikosi kazi cha mashirika mengi kimeamuru ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kuanzisha uchunguzi kuhusu tukio la walimu wakuu wawili wa shule moja huko Laikipia Magharibi nchini Kenya wanaodaiwa kuwafunga wanafunzi watatu kwenye mti kama adhabu. 

Naibu kamishna wa eneo la Nyahururu Moses Muroki Anayekiongoza kikosi kazi hicho alitumia siku ya Jumatano kusikiliza maoni ya walimu na wanafunzi kuhusu tukio hilo lililotolea Ijumaa iliyopita.

Bw. Maina anashutumiwa kuwafunga kwa kamba kwenye mti wanafunzi watatu Ijumaa iliyopita ikiwa ni adhabu kwa kutega shule, kabla ya kuwapiga picha ambazo zilisambaa mitandaoni.

Inadaiwa baadaye alizituma picha hizo kwenye kundi la WhatsApp la walimu kabla ya mmoja wao kuzivujisha picha hizo kwenye mitandao ya kijamii. 

Tukio hilo sasa linafanyiwa uchunguzi na mamlaka zimesema hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi ya walimu hao iwapo watakutwa na hatia.