MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi, Joanfaith Kataraiya,na dereva wake wamenusurika kifo baada ya gari waliyokuwa wakisafiria kupasuka tairi ya mbele ya kushoto na kupinduka  vibaya huko kijiji cha Usangule, Katikati ya kata za Utengule na Mtimbira wilayani Malinyi.

Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Malinyi, Mkuu wa Wilaya hiyo ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, Mathayo Masele, amesema ajali hiyo imetokea  Jana majira ya saa moja kasoro jioni wakati Mkurugenzi huyo akitokea Morogoro Mjini kwenye Vikao kuelekea Malinyi.

Masele amesema walipata taarifa ya ajali hiyo majira ya jioni kutoka Kwa Mkurugenzi mwenyewe baada ya kunusurika na walifika eneo la ajali kijiji cha Usangule,Kilomita 25 kabla ya kufika Malinyi na kilomita saba kutoka Kituo cha afya cha Mtimbira.

Hata hivyo  licha ya maendeleo mazuri ya Mkurugenzi huyo aliyejeruhiwa zaidi miguuni, na Dereva aliyelalamikia kuumia mgongo na kichwa, ajali hiyo ilikuwa ni mbaya Kwa tairi kupasuka na gari kupinduka na tairi kuwa juu na kwamba majira ya saa tano usiku wamewahamishia hospitali ya Rufaa ya St.Francis Ifakara kwa matibabu zaidi  kutoka Kituo cha afya cha Mtimbira  walikokuwa wakipewa matibabu ya awali.

Jitihada zaidi zinaendelea kuupata uongozi wa Hospitali ya St Francis kufahamu taarifa zaidi za kitabibu kuhusu hali ya majeruhi hao.