Shirika la chakula duniani WFP limeonya kwamba mahitaji ya dharura ya chakula kaskazini mwa Ethiopia yanaendelea kuongezeka, wakati ghasia zikienea zaidi ya mipaka ya eneo la Tigray hadi kwenye majimbo jirani ya Afar na Amhara.

Shirika hilo linasema kwamba hadi watu milioni 7 wana uhaba mkubwa sana wa chakula huku wakikabiliwa na baa la njaa. Watu hao ni pamoja na wengine zaidi ya milioni 5.2 walioko jimboni Tigray wanaotegemea msaada wa chakula kutoka Umoja wa mataifa ili kuishi.

WFP inasema kwamba ghasia ambazo sasa zimeenea kwenye eneo lote kaskazini mwa Ethiopia zimesababisha watu wengine milioni 1.7 kukabiliwa na njaa.

Mwezi huu WFP imeanza kupeleka chakula cha dharura kwa watu kaskazini mwa Ethiopia ikiongeza kusema kwamba wanapanga kuwafikia watu laki 5 na 30 (530,000) jimboni Afar pamoja na wengine laki 2 na 50 (250,000 )kwenye jimbo la Amhara.

Wakati huo huo msemaji wa WFP huko Tigary Tomson Phiri amesema kwamba wakati hali ikiendelea kudorora , mashirika ya misaada yanajitahidi kupeleka chakula cha dharura kwa zaidi ya watu milioni 5 kote kwenye jimbo hilo

Phiri ameongeza kwamba WFP imeweza kupeleka malori 355 tu ya misaada tangu katikati ya mwezi Julai.

Amesema kwamba ingawa msaada huo unaonekana kuwa mwingi, ni chini ya asilimia 10 ya msaada unaohitajika jimboni humo, na kwamba malori 100 yanahitajika kila siku huko Tigray ili kukidhi mahitaji.

WFP inaomba ufadhili wa dola milioni 426 ili kuendeleza operesheni ya upelekaji wa misaada kwa takriban watu milioni 12 kote nchini Ethiopia mwaka huu. Shirika hilo limeongeza kusema kwamba litalazimika kukata mgao wa misaada kwa watu wa kaskazini mwa Ethiopia iwapo hawatapata ufadhili zaidi.

Shirika hilo linasema kwamba huenda likasitisha upelekaji wa chakula kwa takriban watu milioni 4 walioko Tigray, Afar na Amhara katika miezi michache ijayo iwapo wataishiwa na fedha.

Novemba 4 mwaka huu itakuwa mwaka mmoja tangu serikali kuu ya Ethiopia ilipoanza operesheni za kijeshi kwa nia ya kumaliza udhibiti wa TPLF kwenye eneo la Tigray.