Mtoto mwenye umri wa miaka mitano (5) aliyefahamika kwa jina la Masule Cosmas  mkazi wa kitongoji cha Mwananghori kijiji cha Zawa , Tarafa ya Sengerema wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu amefariki baada ya kujeruhiwa na fisi huku baadhi ya viungo vyake vya mwili vikiliwa.

Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa polisi Mkoa wa Simiyu Kamishina Msaidizi Richard Abwao amesema kuwa tukio hilo limetukia hana majira ya saa tisa kamili alasiri wakati akiwa na wenzake wakichunga ng'ombe na mbuzi.

Abwao amewataja wenzake aliokuwa akichunga nao ni pamoja na Naomi Amos na Scholastika Wahumija ambapo walikuwa wakichunga kwenye mashamba ambayo yapo mbali kidogo na makazi yao.

Aidha ameongeza kuwa fisi huyo alitokea kwenye kichaka na kuanza kuwakimbiza na kufanikiwa kumkamata na kisha kuanza kula viungo vya mwili wa mtoto huyo ambavyo ni shavu la kulia , na kumtoa ngozi ya kichwa pamoja na macho yote mawili.

Hata hivyo wananchi walimtafuta fisi huyo na baada ya kumpata walimuua na kwamba mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi na daktari na baadae kuukabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya mazishi.

Sambamba na hayo jeshi la polisi Mkoani hapa linatoa wito kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari kwa watoto wao dhidi ya wanyama wakali kwenye maeneo yao hususan vijijini.