Na Amon Mtega, Mbinga.
VIKUNDI Vitatu vinavyojishughulisha na kilimo cha zao la Mahindi katika kata ya Kigonsera na Matiri Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma vimeiomba Serikali kupitia kitengo cha Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula NFRA Mkoani humo kununua mahindi ya vikundi hivyo ili wanavikundi waweze kufanya marejesho ya mikopo wanayodaiwa kwenye taasisi mbalimbali ikiwemo za kwenye mabenki.
Vikundi hivyo ambavyo ni Matiri ,Lingwili na Wadi Mkurumusi vina tani 700 za mahindi ambazo zipo tayari kwa kuuzwa pindi vitakapokuwa vimepatiwa nafasi ya kuuza mahindi hayo.
Akizungumza mmoja wa wanavikundi hao Joyce Hyera amesema kuwa vikundi hivyo vimezalisha mahindi kwa wingi changamoto kubwa ni kupatiwa nafasi ya kuuza kwenye kitengo cha chakula NFRA ambapo hadi sasa hawajui kama watafanikiwa kuuza au hawatafanikiwa.
Joyce ambaye anatokea katika kikundi Cha Lingwili Kigonsera amesema kama vikundi hivyo vitafanikiwa kuuza mahindi hayo kwenye kitengo cha chakula basi watafanikiwa kulipa madeni ambayo walikopa kwenye taasisi mbalimbali zikiwemo za kibenki.
Naye Bonus Mwingira mwenyekiti wa kikundi cha Matiri ameipongeza Serikali kwa kutenga fedha za awamu ya pili takribani Bilioni 50 za kununulia mahindi jambo ambalo linaweza kusaidia vikundi vyao kuuza mahindi ambayo yapo tayari.
![]() |
Baadhi ya wanavikundi wakiwa katika sehemu waliyoweka mahindi huku wakisubiri soko. |
Diwani wa kata ya Kigonsera Simon Komba amesema kuwa vikundi hivi vimekuwa vikijitahidi sana katika suala zima la uzalishaji wa mazao mbalimbali hivyo kama vitafanikiwa kuuza mazao yao ambayo ni mahindi vitatia hamasa na vikundi vingine viweze kuiga mfano huo wa vikundi kufanya kazi.
Kwa mujibu wa diwani Komba amesema awali vikundi hivyo viliahidiwa kuuza mahindi hayo lakini hadi sasa bado vinaendelea kusubiri kupata nafasi ya kuuza mahindi hayo.
![]() |
Diwani wa kata ya Kigonsera Simon Komba akivizungumzia vikundi hivyo juu ya uuzaji mahindi. |
Kwa upande wake Meneja wa NFRA Mkoa wa Ruvuma Ramadhan Nondo amesema ofisi yake inavitambua vikundi hivyo kupitia ofisi ya mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbinga Vijijini hivyo tayari vimewekwa kwenye mpango wa kuhakikisha vinapatiwa nafasi ya kuuza mahindi hayo
Nondo akizungumza kwa simu amesema kuwa lengo la Serikali ni kutaka kila mkulima aweze kunufaika na bei iliyowekwa ya kilo moja shilingi 500 hivyo kufuatia hali hiyo ofisi yake inajitahidi kuona kila namna ya kumnufaisha mkulima katika uuzaji wa mahindi hayo na tayari vitengo vya ununuzi vimepelekwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo na Kigonsera yenyewe.
0 Comments