Mkurugenzi wa mtendaji wa mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Songea (SOUWASA) Patrick Kibasa akizungumzia kuhusu mradi wa maji ambao zaidi ya wakazi 12, 000,watanufaika.

Na.Amon Mtega ,Ruvuma

ZAIDI ya Wakazi 12,000 wa kata tatu katika Halmashauri ya Mji wa Mbinga Mkoani Ruvuma wanatarajia kunufaika na mradi wa Maji ambao umetumia Sh.Bilioni 1.4 ,ambao utakamilika Novemba mwaka huu 2021.

Akizungumza ofisini kwake Mkurugenzi  mtendaji wa mamlaka ya  Maji safi na Usafi wa Mazingira Songea (SOUWASA) Patrick Kibasa amesema kuwa mradi huo unaenda kuondoa changamoto ya upungufu wa maji kwa  wakazi hao ambao kwa muda mrefu walikuwa na changamoto ya upungufu wa maji.

Mkurugenzi Kibasa ambaye ofisi yake inasimamia miradi hiyo kwenye mamlaka ndogo katika Halmashauri ya Mbinga na Tunduru amesema kuwa mradi wa Mbinga  umefikia asilimia 80  na kuwa utahudumia kata tatu ambazo ni Betherehemu ,Luhuwiko na Matarawe.

Kibasa akiuzungumzia mradi wa Mbinga mji amesema kuwa licha ya kuwepo kwa mradi huo unaotarajia kukamilika lakini bado kuna mradi mwingine wa maji ambao utatumia sh.Milioni 700 na kuufanya mji wa Mbinga kuwa na maji ya kutosha kwa asilimia 95 hatimaye kufikia malengo ya Serikali ya awamu ya sita ya kumtua ndoo mama kichwani.

Mkurugenzi huyo amefafanua kuwa miradi hiyo inatekelezwa kwa kutumia mfumo wa Force Account jambo ambalo limesaidia kuokoa fedha nyingi ambazo zingeweza kutumika bila utaratibu.

Kaimu mkurugenzi wa mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira katika mji wa Mbinga(MBIUWASA) James Kida ,akionyesha moja  vituo vya kukusanyia maji vinavyopeleka Tenki kubwa la lenye ujazo wa lita Laki tano(500,000).

Kwa upande wake kaimu Mkurugenzi mtendaji mamlaka ya Maji safi na usafi wa Mazingira katika mji wa Mbinga (MBIWASA) James Kida amesema kuwa mradi huo unaosimamiwa na SOUWASA,Songea utakuwa ukombozi mkubwa kwa wakazi wa mji wa Mbinga.

Kida amesema kuwa mradi huo ambao tenki lake lina ujazo wa lita laki tano (500,000) ambalo limewekwa katika kata ya Betherehemu eneo la Lusaka ,licha ya kuzilenga kata tatu Betherehemu,Luhuwiko na Matarawe lakini bado utawanufaisha wakazi wote wa Mbinga mji kwa kuwa waliokuwa wanapata maji ya bomba walikuwa wakipata kwa mgao lakini sasa mgao hautakuwepo kufuatia kuwepo kwa mradi huo.

Kaimu mkurugenzi huyo ambaye pia ni meneja ufundi amesema kuwa maji hayo yametolewa kwenye vyanzo vinne vya Lupembe ABCD katika kata ya Lwaita na Ndengu Kijiji cha Kiheleketi kata ya Nyoni vyote vinamwaga maji kwenye tenki kubwa lililopo Lusaka kata ya Betherehemu.

Diwani wa kata ya Betherehemu katika Halmashauri ya Mbinga mji ,Amanyisye Ngonepo akiipongeza Serikali pamoja na mbunge wa Jimbo la Mbinga mjini Jonas Mbunda kwa kuufanikisha mradi wa maji Mbinga.

Naye diwani wa kata ya Betherehemu Amanyisye Ngonepo kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi CCM  amesema kuwa wakazi wa kata hizo wameupokea mradi huo kwa mikono miwili huku wakimpongeza mbunge wa Jimbo la Mbinga mjini Jonas Mbunda kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi CCM kwa kuupigania mradi huo kukamilika haraka ili kuondoa adha iliyokuwa ikiwakabili Wananchi hao hasa wakinamama.

Diwani Ngonepo amesema kuwa ofisi ya mkurugenzi wa Mbinga mji pamoja na ofisi ya Mbunge wakishirikiana na wasimamizi wa mradi huo toka SOUWASA ,Songea na MBIUWASA wamefanya kazi kubwa na hatimaye leo wakazi wa Mbinga wananufaika na maji hayo.

Hata hivyo diwani huyo ameipongeza Serikali ya awamu ya sita kwa kuridhia kutoa fedha za kujengea mradi huo na kuwafanya wakazi wa mbinga kuendelea kuwa na imani na serikali yao kutokana na kuthaminiwa kwenye utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ya maji.

Baadhi ya Wakinamama wa kata ya Betherehemu Wilaya ya Mbinga wakichota maji kwenye vituo ambavyo vimekuwa na changamoto kutokana na foleni ya wahitaji huku wakiomba mradi mkubwa ukamilike kwa haraka.

Akizungumza mmoja ya baadhi ya wakinamama wa kata hizo Yosepha Ngindo mkazi wa kata ya Betherehemu ameishukuru Serikali kwa kuwapelekea huduma ya maji ya bomba na kuwa umewaokoa wakinamama kwenye mateso ya  muda mrefu waliyokuwa wakiyapata juu ya ukosefu wa  maji.