Na Hassan Mabuye, Bahi
Kumeibuka tabia kwa wakazi wa maeneo mbalimbali kutojitokeza kuchukua hati zao za umiliki wa ardhi kwa wakati kwa kigezo cha kukwepa kulipa kodi ya pango ya ardhi kitu ambacho kwa sasa Bunge limeipatia muarubaini tabia hii.
Hayo yamesemwa na Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Dodoma Thadei Kabonge wakati akitoa ripoti kwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na maendeleo ya Makazi Dkt Angelina Mabula kuhusu hati ambazo zipo tayari na hazijachukuliwa na Wakazi wa Halmashauri ya Bahi Mkoani Dodoma.
Kabonge ameongeza kuwa mwaka jana Bunge la jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha sheria kwamba ardhi ikishapimwa na ikapita miezi mitatu na mmiliki hajajitokeza kuja kumilikishwa basi itahesabika tayari ushamilikishwa na itaanza kuhesabiwa kodi ya ardhi.
Aidha, Kabonge amewataka wananchi kujitokeza ili kumilikishwa Ardhi kisheria kwa kuwa kutomilikishwa ardhi sio kigezo cha kukwepa kulipa kodi ya ardhi hata kama ardhi hiyo itakuja kumikishwa baada ya miaka kupita.
"Ardhi ikishapimwa ikapita miezi mitatu wewe hujajitokeza kuja kumilikishwa sisi tutahesabu tayari umemilikishwa na inaingia kwenye mfumo wa kudaiwa kodi,huwe na nyaraka huna nyaraka sisi tunajua hii miezi mitatu imeisha lini"amesema Thadei Kabonge.
Amesema hata ikipita miaka kumi baadae na mmiliki wa ardhi atakapokuja kumilikishwa atakuta madai yake ya kodi yapo palepale kwa kuwa tayari anakuwa kaishaingizwa katika kanzi data ya wadaiwa wa kodi ya ardhi tangu siku ya awali hata kama mmiliki hakuwa na hati.
Kamishna Kabonge amebainisha kuwa ofisi yake ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Dodoma ina viwanja zaidi ya 2,550 ambavyo vimepimwa tayari lakini wananchi hawataki kumilikishwa.
0 Comments