Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemfunga kifungo cha nje cha miezi sita aliyekuwa Rais wa Klabu ya Simba, Evans Aveva kwa kosa la matumizi mabaya ya ofisi huku Godfrey Nyange maarufu Kaburu akiachiwa huru baada ya Mahakama hiyo kutomkuta na hatia.

Hukumu hiyo imetolewa leo na Hakimu Mkazi Mkuu,Thomas Simba ambapo amesema hakuna ubishi wowote kuwa Dola za Kimarekani 300,000 zilikuwa zimeingizwa kwenye akaunti ya Klabu ya Simba kupitia Bank ya CRDB ambayo ni mauzo ya mchezaji Emanuel Okwi na baada ya kuingia kwenye kamati tendaji ya klabu ya Simba ilielekeza itolewe fedha hiyo kwenye akaunti ya Simba ili itumike kwenye uwanja wa Bunju kujengea nyasi bandia.

"Mahakama imejitosheleza kuwa ile fedha ilitakiwa ijenge nyasi bandia kwenye uwanja wa Bunju lakini haikufanyika hivyo matokeo yake zilienda kwenye akaunti binafsi ya Aveva"

Hakimu Simba amesema kutokana na mashtaka hayo Nyange hajakutwa na hatia isipokuwa Aveva amekutwa na hatia kwa kutumia nafasi yake vibaya kwa kuingiza fedha hizo kwenye akaunti binafsi ingawa hakuna wizi uliofanyika.
source: Milladayo