NA AMON MTEGA,SONGEA.
WATU watatu wamefariki Dunia kwa ajali ya Bajaji baada ya kugongana na basi la Jeshi la Wananchi katika eneo la Mfaranyaki kwenye barabara kuu ya Mbinga –Songea na kusababisha vifo hivyo akiwemo aliyekuwa mtunza kumbukumbu katika Hospitali ya rufaa ya mkoa wa Ruvuma Devota Challe(60).
Akizungumza ofisini kwake kamanda wa polisi wa mkoa wa Ruvuma Joseph Konyo amelitaja tukio hilo kuwa limetokea Oktoba 11 mwaka huu majira ya saa 12:30 asubuhi huko katika eneo la Mfaranyaki barabara kuu ya Mbinga –Songea na kusababisha vifo hivyo.
Kamanda Konyo licha ya kumtaja marehemu Devota Challe(60) ambaye ni mkazi wa Luhuwiko katika Manispaa ya Songea na alikuwa mtunza kumbukumbu kwenye Hospitali hiyo amewataja marehemu wengine kuwa ni Alei Komba ambaye umri wake haukufahamika mfanyabiashara mkazi wa Matiri Wilaya ya Mbinga na mwingine anayekadiliwa kuwa na umri wa miaka (30-35) ambaye ni wa jinsia ya kike hadi sasa hajatambulika kuwa ni mkazi wa wapi wala jina huku dereva wa bajaji hiyo Alfred Kihwili (Shida) akiwa majeruhi ameumia katika eneo la mwili wake kichwani na shingoni.
Konyo amefafanua kuwa bajaji hiyo yenye namba za usajili MC580 CYD ilikuwa inatokea Luhuwiko ikiwa imebeba abiria hao ambao ni marehemu ilipofika katika maeneo ya Mfaranyaki iligongana na basi la Jeshi linalobeba wafanyakazi lililokuwa likielekea Luhuwiko wakati lilipokuwa likijaribu kuipita gari aina ya Haisi ambapo kabla basi hilo halijamaliza kuipita Haisi hiyo ndipo ghafla likagongana na bajaji hiyo.
Akimzungumzia marehemu Devota Challe kamanda huyo amesema kuwa marehemu huyo alikuwa akienda Hospitalini alikokuwa akifanyia kazi kwa lengo la kwenda kuwaaga watumishi wenzake kwa kuwa alikuwa amepatiwa barua ya kustaafu na alipokuwa amepanda bajaji hiyo yeye na abiria wenzake walipatwa na ajali hiyo kisha kupoteza maisha.
Kamanda huyo ametoa wito kwa madereva wa vyombo vya moto kuwa makini wanapokuwa barabarani hasa madereva wa magari makubwa wamekuwa wakijivunia ukubwa wa magari yao na kuwasababishia ajali wenye magari madogo ,Pikipiki,na Bajaji .
0 Comments