KAMPUNI YA MANTRA YATOA MSAADA KWA WANAFUNZI WALEMAVU,NAMTUMBO.




Na Amon Mtega, Namtumbo.

WATOTO wenye matatizo ya ulemavu mbalimbali wakiwemo wenye matatizo ya kuona wanaosoma katika shule ya msingi ya Namtumbo Mkoani Ruvuma wamepatiwa vifaa mbalimbali ikiwemo fimbo za kutembelea kutoka kwenye kampuni ya Mantra Tanzania inayohusika na madini ya Uranium katika mto Mkuju uliopo Wilayani humo ili kuwapunguzia changamoto zinazowakabili watoto hao.

Afisa elimu wa kitengo maalum wa Wilaya ya Namtumbo Thabiti Mponda ameishukuru kampuni ya Mantra Tanzania kwa msaada huo amesema kuwa vifaa hivyo vitawasaidia kupunguza adha iliyokuwa ikiwakabili watoto hao hasa wanapokuwa kwenye masomo kutokana na upungufu wa vifaa vya mahitaji yao vikiwemo vya kujifunzia.


Mponda amesema kuwa katika Wilaya hiyo watoto wenye ulemavu wanafikia 480 lakini waliofanikiwa kupelekwa shule ni wachache kutokana na changamoto za shule kukosa mabweni ya kukaa watoto hao jambo ambalo hupelekea watoto wengine wenye ulemavu kushindwa kupata fursa ya elimu.

Afisa elimu huyo amefafanua kuwa katika Wilaya hiyo kuna vituo vinne ambavyo ni Namtumbo,Lusewa ,Nambehe na Karume ambavyo vyote vinakabiliwa na changamoto zinazofanana hivyo amewaomba wadau mbalimbali kujitokeza kama ilivyofanya kampuni ya Mantra Tanzania ambayo hadi sasa zaidi ya sh, Milioni kumi na moja(11) zimetumika kuhudumia vifaa vya watu wenye ulemavu mbalimbali wakiwemo wanafunzi wenye ulemavu.

Kwa upande wake mwalimu mkuu wa kitengo maalum katika shule ya msingi Namtumbo Bibiana Buvanza amesema kuwa kumekuwepo na changamoto kubwa ya upungufu wa vifaa vya kujifunzia watoto hao ukilinganisha na idadi ya wanafunzi waliopo ambao 46 Viziwi tisa,  Asiyeona mmoja ,Usonji watatu na Ulemavu wa Akili 33 toka hatua ya kwanza hadi ya tatu.


Naye Afisa elimu msingi katika Halmashauri ya Namtumbo Lulu Mapunda amesema kuwa msaada uliotolewa na kampuni ya Mantra Tanzania utasaidia kutoa hamasa ya uelewa kwa watoto hao kujifunza zaidi pamoja na kuwapa hamasa Walimu kutokana na uwepo wa baadhi ya vifaa hivyo ambavyo awali vilikuwa shida kuvipata.

Ofisa mahusiano wa kampuni ya Mantra Tanzania Khadija Pallangyo amesema kuwa kampuni hiyo imekuwa ikisaidiana na jamii katika kutatua changamoto mbalimbali ikiwemo na ya watu wenye ulemavu kwa kuwapatia mahitaji mbalimbali ya vifaa ili kuwapunguzia changamoto zinazowakabili na kuenda sambamba na Serikali ya awamu ya sita ya kuyajali makundi maalum wakiwemo walemavu.


Pallangyo amesema kuwa kampuni hiyo inayotarajia kuanza kuchimbwa hivi karibuni baada ya taratibu kukamilika itaendelea kushirikiana na jamii katika kutatua changamoto mbalimbali za kwenye jamii hizo ili mwisho wa siku kufikia malengo yaliyokusudiwa na kuwa hadi sasa kwa upande wa kundi la walemavu wametoa vifaa vya kuwasaidia kusikia kwa wale viziwi, imetoka baiskeli kwa mlemavu mmoja wa miguu ,fimbo mbili katika shule ya msingi Namtumbo ambayo fimbo moja amepewa mwanafunzi Muntazari Sanane mlemavu macho,pamoja na vifaa vya kusomea alama nundu.

Post a Comment

0 Comments