Diwani wa kata ya Kitanda Aureus Ngonyani akiwataka Viongozi wa CCM wa kata hiyo kushirikiana na watendaji wa Serikali ili kufanikisha kutekeleza miradi kwa wakati.


Na Amon Mtega , Mbinga.

DIWANI wa Kata ya Kitanda Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi CCM Aureus Ngonyani amewataka Vijana wa kata hiyo kuendelea kujitoa kufanya kazi za maendeleo ili kujiongezea kipato cha mtu mmoja mmoja na kata kwa ujumla.

Ngonyani ameutoa wito huo wakati wa kikao cha Halmashauri kuu ya CCM kata ambacho ni maalum kwaajili ya kujadili maendeleo ya kata hiyo katika kipindi cha mwaka mmoja tangu aingie madarakani .

Akizungumza kwenye mkutano huo ambao mgeni rasmi alikuwa Mjumbe wa Sekretarieti ya Wilaya ya Mbinga Angelo Madundo diwani huyo amesema kuwa kama  Vijana watajituma katika kufanya kazi za maendeleo basi pato la mtu mmoja mmoja litaongezeka.


Diwani huyo akizungumzia upande wa utekelezaji wa miradi amesema kuwa hadi sasa miradi mbalimbali imetekelezwa na mingine bado inaendelea kutekelezwa huku akiwaomba Viongozi wa CCM waendelee kushirikiana na watendaji wa Serikali ili kufanikisha kwenda kasi zaidi kwenye utekelezaji wa miradi hiyo.

Kwa upande wake mjumbe wa Sekretarieti ya Wilaya ya Mbinga Angelo Madundo amesema kuwa taarifa nyingi za miradi zinazojadiliwa kwenye kata inatakiwa zianze ngazi ya ngazi ya chini kwenye Vijiji ili ikifika kwenye kata kila mmoja anakuwa anauelewa.

Mjumbe wa sekeletarieti ambaye pia ni katibu wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM Wilaya ya Mbinga Angelo Madundo akizungumza kwenye mkutano wa Halmashauri kuu ya kata ya Kitanda Wilayani humo.

Madundo ambaye pia ni katibu wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM Wilaya ya Mbinga amesema kuwa kumekuwepo na baadhi ya wenyeviti wa Vijiji kushindwa kushirikiana na Viongozi wa CCM wa matawi kuungana kupita kuangalia miradi inayotekelezwa jambo ambalo mwisho wa siku Viongozi wanatazama kuhusu miradi hiyo.

Mjumbe huyo ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye mkutano huo amesema kuanzia sasa Viongozi wa Chama na Serikali wanatakiwa kwenda kushirikiana ili mambo yazidi kusonga mbele kimaendeleo.


Hata hivyo Madundo amempongeza diwani Aureus Ngonyani wa kata hiyo pamoja na mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbinga mji Grace Quintine kwa kazi kubwa za kusimamia ilani ya chama Cha Mapinduzi CCM ambayo fedha zake zinatolewa na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Mtendaji wa kata ya Kitanda Festo Komba akisoma taarifa ya utekelezaji wa maendeleo ya miradi ya kata hiyo.
Naye Afisa mtendaji wa kata ya Kitanda Festo Komba wakati akisoma taarifa ya utekelezaji wa miradi mbalimbali kwenye kata hiyo amesema kuwa Diwani wa kata hiyo amekuwa halali katika kutekeleza majukumu ya Wananchi na kuwa katika miradi aliyoipigania ni pamoja na kuhakikisha umeme wa Rea Vijijini unatakiwa kufika kwenye kata hiyo na kusambaza kwenye Vijiji vitano vilivyopo kwenye kata hiyo.