Maisha ya  ndoa yana changamoto nyingi sana ambazo wanandoa hukabiliana nazo.

Katika kipindi  cha misukosuko ya ndoa mwanamke au mwanaume epuka kuwashirikisha wanafamilia wako kila changamoto ya mwenzi wako unayokumbana nayo kwani kuna makosa ambayo itafika wakati wewe unaweza kumsamehe mwenzi wako lakini wanafamilia wako wakashindwa kumsamehe.

Maisha ya ndoa ni kiapo cha watu wawili walioahidiana mbele ya kadamnasi kuvumiliana katika shida na raha hivyo hata kama kuna jambo limewazidia kulitatua wenyewe basi mnaposhirikisha familia kuweni makini katika uwasilishaji wake kwani kila mmoja ana uelewa wake na hisia zake  katika kulipokea jambo hilo.

Epuka kuwashirikisha matatizo yako ya ndoa wanafamilia wako wakati umejawa na jazba na hasira kwa mwenzi wako ipo haja ya kutulia na kutafakari kabla hujaamua kuwashirikisha kwani hasira na jazba hutawaliwa na maneno mengi usipokuwa makini unaweza ukaongea hata ambayo hawakupaswa kuyajua kuhusu mwenza wako na ndipo chuki huanzia hapo baina ya ndugu na mwenzi wako.

Changamoto katika ndoa haziepukiki cha msingi ni wewe unaamua kuzipa nafasi ipi katika ndoa yako ni jambo la kuchagua kama ndoa yako iwe mikononi mwako na Mungu wako  au iwe mikononi mwa ndugu na rafiki zako kwamba kila jambo unawashirikisha haijalishi lina uzito gani.

Sio kwamba ndugu hawapaswi kujua mapito ya ndoa yenu ila unapaswa kupima ni yapi wayajue na yapi wasiyajue ili kuzidi kulinda heshima yako na ya mwenzi wako kama huwezi kumuacha kwa changamoto hizo .

Ushauri

Katika maisha ya ndoa baadhi ya mambo muhimu ya kuzingatia ni kuheshimiana, kujaliana, kuvumiliana,kuaminiana n.k endapo haya yatapata nafasi kubwa katika ndoa yenu basi amani na upendo na furaha vitatawala nyumbani mwenu kiasi kwamba hata changamoto ikijitokeza inakuwa rahisi kuitatua.