Mgeni rasmi Mbassa Sanga akizungumza kwenye mahafali ya kidato cha Nne katika Sekondari ya Mkinga.

Amon Mtega, Mbinga.

MWENYEKITI wa bodi ya Shule ya Sekondari ya Mpoloto iliyopo jiji la Mbeya, Mbassa Sanga ameipongeza Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi CCM ya Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma kwa kuisimamia Sekondari ya Mkinga na kuifanya iendelee kuwa na ufaulu mzuri kwa wanafunzi.

Pongezi hizo amezitoa wakati akizungumza kwenye mahafali ya kidato cha Nne ya shule hiyo ambayo wahitimu wapo 42 na imehudhuriwa na watu mbalimbali wakiwemo Wazazi wa wahitimu pamoja na Viongozi wa chama na Serikali .


Mwenyekiti Sanga ambaye amekuwa mgeni rasmi kwenye mahafali hayo amesema kuwa ni ukweli usiopingika Jumuiya ya Wazazi ya Wilaya ya Mbinga kwa kushirikiana na mkuu wa shule hiyo Jacob Msigwa wameirudisha Sekondari hiyo kwenye hadhi yake na kuifanya iwe ni moja ya shule zenye ushindani wa kitaaluma.

Wanafunzi wahitimu wa Sekondari ya Mkinga Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma wakimuomba Mungu awajalie katika mitihani yao .

Hata hivyo mgeni rasmi huyo baada ya kusomewa baadhi ya changamoto hasa ya umaliziaji wa jengo la utawala, kuweka marumalu chini amechangia fedha ya boksi 12 na huku akiwataka na wazalendo wengine kuunga mkono ambapo Jumuiya ya Wazazi ikiongozwa na mwenyekiti Erenest Mjirima (Mgogo) imetoa sh.100,000=na hitaji la marumalu ni boksi 80.


Aidha mwenyekiti Sanga ameipongeza shule hiyo kwa kuongeza kidato cha tano na sita (HIGH SCHOOL)jambo ambalo amesema litazidi kuongeza ushindani mkubwa katika ongezeko la taaluma huku akiwataka wahitimu wa kidato cha Nne kutumia fursa ya shule hiyo kujiunga kidato cha tano na sita.

Mkuu wa shule ya Sekondari ya Mkinga Jacob Msigwa akizungumzia mafanikio ya shule hiyo pamoja na changamoto zilizopo.

  Kwa upande wake mkuu wa shule hiyo Jacob Msigwa wakati akitoa taarifa ya shule hiyo amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo shule hiyo imefanya vizuri kwenye taaluma na kuifanya iwe na ufaulu wa asilimia 100 jambo ambalo amesema limesaidia kuendelea kuipandisha Sekondari hiyo.


 Msigwa amesema kuwa kumekuwepo na changamoto mbalimbali za kimiundombinu ambazo baadhi zinaendelea kutatuliwa kwa kushirikiana na Jumuiya ya Wazazi wa CCM ikiwemo umaliziaji wa jengo la utawala.

Mkuu wa shule ya Sekondari ya Mkinga Jacob Msigwa akizungumzia mafanikio ya shule hiyo pamoja na changamoto zilizopo.

  Naye mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Mbinga Mkoani humo Erenest Mjirima amewataka Wazazi wa wahitimu hao kufanya jitihada za kuwaendeleza kimasomo wanafunzi hao na kuachana na tabia ya kukimbilia kupokea posa za kutaka waolewe au waoe jambo ambalo hurudisha maendeleo ya watoto.


 "Kuna tabia kwa baadhi ya wazazi wakishaona mtoto kahitimu kidato cha Nne basi anajiona amemaliza kazi na kufikiria kupokea posa za wanaume au kama ni kijana wakiume kumtaka aoe nasema marufuku "amesema mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM Wilaya ya Mbinga Erenest Mjirima.


 Pia katibu wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Mbinga Angelo Madundo akizungumza mara baada ya mahafali hayo amesema kuwa Jumuiya hiyo ipo imara na kuwa itaendelea kushirikiana na Walimu wa shule hiyo ili kufanikisha kukamilisha miundombinu iliyobakia.