Mkurugenzi wa kampuni ya LOHE Tanzania Limited,Longinus Komba akizungumza kwenye mahafali ya shule ya Sekondari ya Ngwilizi. |
Na Amon Mtega, Mbinga.
MKURUGENZI wa Kampuni ya LOHE Tanzania Limited ,Longinus Komba amewataka wahitimu wa kidato cha Nne wa shule ya Sekondari ya Ngwilizi iliyopo kata ya Kitanda Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma ,kwenda kutumia vema Elimu waliyoipata shuleni ili kufanikisha kukabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo ya ajira.
Wito huo umetolewa na mkurugenzi wa Kampuni hiyo yenye makao yake makuu Wilaya ya Mbinga wakati wa mahafali ya kumi na Nne (14) ya shule hiyo alipoalikwa kuwa mgeni rasmi kwenye mahafali hayo ambayo yamehudhuriwa na watu mbalimbali wakiwemo Viongozi wa vyama vya siasa na Serikali.
Komba amesema kuwa kumekuwepo kwa baadhi ya wahitimu kushindwa kutumia Elimu waliyoipata ipasavyo jambo ambalo hupelekea kuona maisha magumu na hatimaye hujiingiza kwenye vitendo viovu na mwisho wa siku maisha yao huharibika.Mkurugenzi wa Kampuni hiyo inayojishughulisha na mambo mbalimbali ikiwemo uchakataji wa unga wa mahindi( sembe ) licha ya kuwaasa wahitimu hao lakini kampuni yake imetoa msaada wa Komputa sita(6)ambazo zimeunganishwa na mtandao (Internet)ili kuwafanya wanafunzi waweze kuwa na uelewa zaidi katika ulimwengu wa Sayansi na Teknolojia.
Mgeni rasmi huyo ambaye naye alisoma shule hiyo licha ya kutoa msaada wa Komputa hizo lakini ameahidi kuongeza miche ya miparachichi ili iweze kuongezea kasi ya upandaji wa matunda hayo kwenye eneo la shule na kisha kuyafanya mazingira yaendelee kuhifadhiwa.
Hata hivyo kampuni yake pia imeahidi kutoa msaada wa Runinga (TV) ya kisasa kwa matumizi ya Walimu na shule ili kuwaondolea adha ya kwenda umbali mrefu kupata huduma ya upataji habari mbalimbali za kitaifa na kimataifa.
Kwa upande wake mkuu wa shule hiyo Giliadi Mabena awali akisoma taarifa ya shule hiyo amesema kuwa shule hiyo licha ya kuwa na ufaulu mzuri lakini inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa samani za ofisini katika ofisi ya mwalimu mkuu na ofisi za walimu.
Mabena licha ya shule hiyo kukabiliwa na changamoto hizo lakini ameipongeza kampuni ya LOHE Tanzania Limited kupitia mkurugenzi wake Longinus Komba kwa msaada mkubwa anaoutoa shuleni hapo ambapo hadi sasa ameshatoa msaada wa zaidi ya kilo 700 za unga wa sembe kwaajili ya chakula cha wanafunzi shuleni hapo jambo ambalo hupelekea kupunguza utoro kwa wanafunzi hao.
Diwani wa kata ya Kitanda Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma Aureus Ngonyani akiwataka Wananchi kuendelea kuchukua tahadhari juu ya ugonjwa wa Corona,wakati wa mahafali ya shule ya Sekondari ya Ngwilizi. |
Naye diwani wa kata ya Kitanda Aureus Ngonyani wakati wa mahafali hayo ametumia nafasi hiyo kuwataka Wananchi waendelee kuchukua tahadhari juu ya ugonjwa wa Corona pamoja na kujiandaa kuhesabiwa kwenye Sensa itakayofanyika mwakani 2022.
0 Comments