Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Rwanda Leo imetiliana saini ya hati ya makubaliano ya ushirikiano katika masuala ya ulinzi.
Mkataba huo umesainiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Liberata Mulamula (mb) na kwa upande wa Serikali ya Jamuhuri ya Rwanda uliongozwa na Mhe. Vicent Biruta Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam katika Mkutano wa 15 wa Tume ya pamoja ya ushirikiano wa kudumu (JPC), Waziri Mulamula amesema kuwa, awali Mkutano ulipitia taarifa ya makubaliano yaliofanyika katika Mkutano wa 14 wa tume ya pamoja ya ushirikiano wa kudumu.
Amesema kuwa, makubaliano hayo yaligawanywa katika makundi Makuu matatu, ikiwemo Siasa na Mashauriano ya kidiplomasia, Uchukuzi na Miundombinu pamoja na Biashara na Viwanda.
"Kwa upande wa mashauriano ya kidiplomasia ilihusisha ushirikiano wa vyuo vya diplomasia pamoja kamati ya kuratibu utekelezaji wa makubaliano yaliofikiwa, ambapo kwa Uchukuzi na Miundombinu ilihusisha Maendeleo ya Miundombinu na Uchukuzi pamoja na masuala ya Fedha"amesema Waziri Mulamula.
Ameongeza kuwa, kwa upande wa Biashara na Viwanda ilihusisha Sekta za Biashara, viwanda, Uwekezaji, Nishati,Utalii,Kilimo na Teknolojia ya Mawasiliano ya Habari.
Aidha amesema pande zote mbili zilijadiliana na kukubaliana kuhusu maeneo mapya ya ushirikiano yaliopendekezwa, ambapo miongoni mwa maeneo hayo ni manunuzi ya umeme kutoka mrafi wa RASUMO, ushirikiano katika uchimbaji wa petrol na gesi na kubadilishana wanafunzi katika chuo Cha diplomasia Cha Tanzania (CFR) na chuo Cha diplomasia Cha Rwanda kitakacho anzishwa mwaka 2022.
Vile vile amesema Wizara na Taasisi za nchi hizo zinazohusika na rasimu za mikataba ambayo haijasainiwa , zimeelekezwa kuhakikisha zimakamilisha mchakato wa kukamilika rasimu hizo ili kusainiwa.
0 Comments