KATIBU wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma Angelo Madundo amewataka Wajasiriamali wa kikundi cha Amani kilichopo Kijiji cha Matekela kata ya Kambarage kwenda kutumia vema fedha kiasi Cha Sh.Milioni Saba(7,000,000) walizokopeshwa na Halmashauri ili kufikia malengo yaliyokusudiwa na Serikali ya kuwainua kiuchumi Wananchi kupitia vikundi.
Madundo ametoa wito huo ofisini kwake wakati Uongozi wa kikundi hicho ulipoenda kumshukuru kwa kuwasimamia kuwawezesha kupatiwa mkopo huo kutoka katika Halmashauri ya Mbinga Vijijini Mkoani humo ambao wamedai kuwa utawasaidia kufikia malengo.
Katibu huyo amesema kumekuwepo na baadhi ya vikundi ambavyo vikifanikiwa kupatiwa mkopo basi mkopo huo unaishia kwenye mifuko ya Viongozi bila kufanya malengo waliyojipangia wanakikundi jambo ambalo hupelekea migogoro na kufanya mkopo kushindwa kurejeshwa kwa wakati .
Kwa upande wake katibu wa kikundi hicho Petro Nzuyu amemshukuru katibu wa Jumuiya ya Wazazi huku akiahidi kuwa wataenda kufanyia malengo yaliyokusudiwa ya kufunga kinu cha kuchakatia unga wa mahindi ' Sembe' ambao utauzwa maeneo mbalimbali ndani na Nje ya Kijiji.
![]() |
Afisa maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Mbinga Vijijini Justiner Sigera awali alipokuwa amekitembelea kikundi hicho na kisha kupeana majukumu ya kuyafanya kabla ya kupatiwa mkopo huo. |
Nzuyu pia amemshukuru afisa maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Mbinga Vijijini Justiner Sigera kwa kukitembelea kikundi hicho na kuona kina sifa ya kupatiwa mkopo huo jambo ambalo amesema linawafanya wanakikundi hicho kuchapa kazi kwa bidii.
Kikundi hicho ambacho kimeundwa na Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi CCM katika Kijiji hicho kinajishughulisha pia na ufugaji Ng'ombe,Mbuzi,Kuku,Sungura pamoja na upandaji miti na sasa kinaongeza mradi mwingine wa kuchakata unga wa mahindi kufuatia mkopo waliopatiwa.
0 Comments