Na. Amon Mtega ,Namtumbo.
AFISA Elimu ya watu wazima katika Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma Shaibu Majiwa ameipongeza kampuni ya Mantra Tanzania L.T.D ,inayojihusisha na mradi wa madini ya Uranium katika mto Mkuju uliyopo Wilaya ya Namtumbo mkoani humo kwa ufadhili wa vitu mbalimbali kwenye jamii ikiwemo masuala ya Elimu ,Afya jambo ambalo limesaidia kupunguza baadhi ya changamoto kwenye jamii ambazo zilikuwa zikiwakabili.
Pongezi hizo amezitoa wakati akifungua maktaba yenye thamani ya zaidi ya Sh, Milioni 22 iliyotolewa na kampuni ya Mantra Tanzania katika shule ya Sekondari ya Wavulana iitwayo Pamoja iliyopo Wilayani humo ambayo inachukua kidato cha tano na sita.
Akifungua maktaba hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Namtumbo Chiriku Chilumba na kuikabidhi shule hiyo kwaajili ya wanafunzi kuanza kujisomea Afisa Elimu Majiwa amesema kuwa amejionea ubora wa maktaba hiyo ambayo ni ya kisasa jambo ambalo litawafanya wanafunzi waweze kuongeza ufaulu wao huku akiutaka uongozi wa shule hiyo kuitunza maktaba hiyo.
Kwa upande wake Meneja Uhusiano wa kampuni ya Mantra Tanzania Khadija Pallangyo amesema kuwa kampuni hiyo imeshatoa ufadhili mbalimbali kwenye jamii ikiwemo mashuleni kwa kuwawekea maktaba za kisasa (ELEKTRONIKI) na kuwa hadi sasa shule za Sekondari saba za Wilayani humo zimewekwa maktaba ambapo shule tatu maktaba za kawaida na shule Nne maktaba za Kielektroniki.
Pallangyo amefafanua tangu kuanza kuweka maktaba kwenye shule hizo kampuni imeshatumia zaidi ya Sh,Milioni 100 ukiachana na ufadhili wa kwenye Afya pamoja na visima vya maji kwenye baadhi ya shule.
Mkuu wa shule ya Sekondari ya Pamoja Amos Mapunda akizungumzia baadhi ya changamoto za shule hiyo ikiwemo upungufu wa mabweni na ukumbi wa mikutano. |
Naye mkuu wa shule hiyo Amos Mapunda akiipokea maktaba hiyo amesema kuwa ni msaada mkubwa kwa kuwa shule hiyo imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa maktaba jambo ambalo kwa sasa limeshatatuliwa na kampuni ya Mantra.
Mmoja wa wanafunzi wa Sekondari ya Pamoja Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma akitumia Kompyuta kwenye maktaba iliyotolewa msaada na kampuni ya Mantra muda mfupi baada ya kuizindua . |
Hata hivyo mwanafunzi Shaibu Shaibu wa kidato cha sita amesema kuwa kuwepo kwa maktaba hiyo ya kisasa yenye Kompyuta zilizounganishwa na mtandao (Internet) kutawasaidia kuwa na uelewa zaidi na kufanya waweze kuongeza ufaulu.
0 Comments