Na Amon Mtega,Manyoni.
VIJANA 50 wa Wilaya ya Manyoni Mkoani Singida ambao walikuwa katika mazingira hatarishi (Duni) wamehitimu mafunzo ya ufundi wa fani mbalimbali kwa ufadhili wa Mbunge wa Jimbo la Manyoni mashariki Dkt Pius Chaya.
Akizungumza na mtandao huu katibu wa mbunge wa Jimbo hilo Tumaini Kalikule amesema kuwa Vijana hao ambao waliibuliwa kwenye kata 19 za Jimbo hilo kwa kila kata kuchukuliwa Vijana wawili (2) hadi (3) kulingana na ukubwa wa kata wamehitimu mafunzo hayo katika chuo Cha ufundi stadi (VETA) kinachomilikiwa na Kanisa la Romani Katholiki Jimbo la Manyoni.
Kalikule amesema kuwa ufadhili huo uliotolewa na Mbunge huyo ni wa Sh.51 milioni ambazo zimetoka mfukoni mwake na siyo fedha za Jimbo kama baadhi ya watu wanavyodhania.
Huo ni moja ya muonekano wa furaha ya kuhitimu mafunzo ya ufundi stadi VETA kufuatia msaada wa Mbunge wa Jimbo la Manyoni mashariki Dkt Pius Chaya. |
Amesema kuwa mafunzo ya vijana hao yenye fani mbalimbali kama Ushonaji,Udereva wa vyombo vya moto(Gari) ufundi magari pamoja na ufundi umeme yafanyika kwa miezi tisa kuanzia Februari 2021.
Katibu huyo amefafanua kuwa gharama hizo zinatokana na kulipa Ada ,Chakula, Hosteli ,Sare pamoja na kulipia maji na umeme kwa kipindi chote wakiwa kwenye mafunzo hayo.Aidha amesema kuwa licha ya Mbunge Dkt Pius Chaya kuwafadhili vijana hao lakini bado anawasomesha wengi wa Jimbo hilo kwenye vyuo ikiwemo vyuo vikuu waliokosa mikopo ili kuendana sambamba na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha jamii inaboreshwa maisha yao.
Mmoja wa Wazazi Betha Samweli akimshukuru Mbunge wa Jimbo la Manyoni mashariki Dkt Pius Chaya kwa jinsi anavyojitolea kutoa misaada mbalimbali kwenye Jamii. |
Kwa upande wake mmoja wa Wazazi kutoka Jimbo hilo Betha Samweli amesema akizungumza kwa niaba ya Wazazi wenzake amemshukuru Mbunge wa Jimbo hilo huku akimuombea kwa Mungu aendelee kuwaangalia watoto wanaotokea katika mazingira hatarishi ili waweze siku za baadae kuishi katika mazingira mazuri ya kujitegemea .
0 Comments