Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma Pili Mande akizungumza na baadhi ya waandishi wa Habari wa mkoa huo kufuatia wanaume wawili kuua wake zao kwa wivu wa kimapenzi.
Na Amon Mtega, Ruvuma
JESHI la polisi mkoani Ruvuma linawasaka watu wawili katika matukio tofauti kwa tuhuma za kuwashambulia kwa vipigo wake zao na kuwasababishia vifo.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Pili Mande amelitaja tukio la kwanza limetokea Oktoba 31 mwaka huu majira ya mchana huko katika Mtaa wa Mateka manispaa ya Songea.
Mande amesema kuwa inadaiwa kuwa Marehemu huyo ambaye jina lake limehifadhiwa kabla ya kifo chake alikuwa kwenye sherehe nyumba ya jirani yao akiwa amesimama na mwanaume mwingine kwenye sherehe hiyo na ndipo alipokutwa na mme wake ambaye naye jina limehifadhiwa kwa sababu za kiuchunguzi zaidi.
Amesema kuwa baada ya kukutwa na mume wake huyo akiwa amesimama na mwanaume mwingine alianza kumshambulia kwa kumshushia kipigo katika maeneo mbalimbali ya mwili na kumsababishia Bandama kupasuka jambo ambalo lilipelekea kuvuja kwa damu nyingi hadi kifo kutokea.
Baadhi ya waandishi wa Habari wa Mkoani Ruvuma wakimsikiliza kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma Pili Mande wakati akizungumzia juu wanaume wawili kuua wake zao kwa wivu wa kimapenzi.
Kamanda Mande alifafanua kuwa inadaiwa mtuhumiwa baada ya kumshushia kipigo mke wake na kugundua kuwa ameua alimchukua mtoto wake na kwenda kumtelekeza kwa baba yake mzazi ambaye jina lake limehifadhiwa kisha baadae alikimbia na kutokomea kusikojulikana.
Aidha kaimu kamanda Mande amelitaja tukio la pili kuwa limetokea Oktoba 28 mwaka huu majira ya usiku huko katika kijiji cha Mageuzi Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma ambapo mwanamke mmoja ambaye jina lake halikutajwa mwenye umri wa miaka 33 inadaiwa kuwa alipigwa na shoka kichwani kutokana na mume wake kumtuhumu kuwa ana mahusiano ya kimapenzi na wanaume wengine.
Alieleza kuwa wapenzi hao walikuwa wametengana lakini siku ya tukio bwana alimlaghai mpenzi wake wa kike kwa kumywesha pombe kisha kwenda nae nyumbani kwake ambako baadae alimshambulia kwa kumpiga na shoka kichwani na kumsababishia kifo.
Mtuhumiwa baada ya tukio hilo inadaiwa kuwa aliuza mahindi na maharage ambayo alipata nauli kisha alikimbia na kutokomea kusiko julikana na polisi inaendelea kumsaka.
Jeshi la polisi kutokana na matukio hayo kukithiri mkoani humo limekemea na kulaani vikali kwa mtu yeyote atakayebainika kumshambulia kwa kumpiga mke wake au mume wake atachukuliwa hatua kali za kisheria bila kujali wadhifa wake kwa kuwa mashambulio hayo yanaleta madhara makubwa kwa familia na jamii kwa ujumla na si vinginevyo.
Katika hatua myimgine kaimu kamanda Mande amesema kuwa kwa wale wanaomiliki silaha kinyume cha sheria amewataka wajisalimishe wenyewe kwenye vituo vya polisi vilivyopo jirani kuanzia Novemba mosi hadi Novemba 30 mwaka huu.
0 Comments