WAJUMBE HALMASHAURI KUU YA CCM KATA KITANDA-MBINGA WAISHUKURU KAMPUNI YA LOHE TANZANIA LTD KWA MSAADA WA KOMPYUTA.

Diwani wa kata ya Kitanda Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma,Aureus Ngonyani akizungumzia umuhimu wa mafunzo ya Kompyuta kwa mwanafunzi wa Sekondari.


Na.Amon Mtega,Mbinga.

BAADHI ya  Wajumbe wa Halmashauri kuu ya Chama cha Mapinduzi CCM ,Kata ya Kitanda Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma wameishukuru kampuni ya Lohe Tanzania Limited ,kwa kutoa msaada wa Kompyuta sita katika shule ya Sekondari ya Ngwilizi iliyopo katani hapo .

Akizungumza mmoja wa wajumbe hao Otilia Ndimbo wakati wa mkutano wa Halmashauri kuu  ya kata hiyo wa kujadili utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa muda wa mwaka mmoja tangu uchaguzi mkuu ufanyike.


Wakati wakijadili taarifa ya utekelezaji wa ilani hiyo juu ya maendeleo ya miradi mbalimbali iliyofanyika kwenye kata hiyo Ndimbo amesema kuwa kuna maendeleo makubwa yanafanyika katika kata hiyo ikiwemo na kwenye shule ya Sekondari ya Ngwilizi kupatiwa Kompyuta sita za kisasa zilizounganishwa na mtandao (INTERNET).

Kwa upande wake diwani wa kata hiyo Aureus Ngonyani amesema kuwa kampuni hiyo ilitoa msaada wa Kompyuta hizo wakati wa siku ya mahafali ya kidato cha Nne yaliyofanyika shuleni hapo kufuatia ahadi ambayo ilitolewa siku za nyuma na mkurugenzi wa kampuni hiyo Longinus Komba .

Diwani huyo amesema kuwa wanafunzi wakisoma na masomo ya Kompyuta yatawafanya wawe na uelewa zaidi utakaowasaidia kuongeza ufaulu zaidi katika masomo yao.

Naye mjumbe wa sekretarieti wa chama cha mapinduzi CCM Wilaya ya Mbinga Angelo Madundo amewataka wajumbe hao kuwaunga mkono wadau mbalimbali wanaojitokeza kufanya maendeleo kwenye jamii kama ilivyofanya kampuni ya Lohe Tanzania Limited.

Mjumbe wa Sekretarieti ambaye pia ni katibu wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma Angelo Madundo akizungumzia umuhimu wa kuwaunga mkono wadau wa mbalimbali wanaojitolea kuleta maendeleo kwenye jamii.


Madundo ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye mkutano huo ambae pia ni katibu wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM ,Wilaya ya Mbinga amesema kuwa wadau ambao wamekuwa wakisaidia maendeleo katika maeneo mbalimbali ikiwemo Mbinga wamekuwa wakienda sambamba na mpango wa Serikali wa awamu ya sita ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwaletea maendeleo Wananchi wake.


Kampuni hiyo yenye makao yake makuu Wilaya ya Mbinga ambayo inajishughulisha na kazi mbalimbali ikiwemo uchakataji wa Sembe Wilayani humo licha ya utoaji wa Kompyuta hizo lakini imeshatoa msaada kwenye shule hiyo miche ya miparachichi zaidi ya mia moja ili kulinda mazingira ya shule hiyo pamoja na kukuza uchumi pamoja na unga wa sembe mifuko 25 yenye kilo 25 kwaajili ya chakula cha wanafunzi hao.

Mkurugenzi wa kampuni ya LOHE Tanzania Limited Longinus Komba akikabidhi Kompyuta sita kwaajili ya matumizi kwa wafunzi wa shule ya Sekondari ya Ngwilizi iliyopo kata ya Kitanda Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma


Post a Comment

0 Comments