Na Amon Mtega,Songea.
BAADHI ya Wananchi wa Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wameipongeza Mamlaka ya maji safi na usafi wa Mazingira (SOUWASA) kwa kuboresha upatikanaji wa maji ikilinganishwa na miaka ya nyuma licha ya kuwepo kwa mabadiliko ya tabia Nchi.
Suzana kapinga mkazi wa Mtaa wa Makambi kata ya Ndilima Litembo Manispaa ya Songea amesema kuwa hali ya upatikanaji wa maji mwaka huu umekuwa mzuri ukilinganishwa na miaka ya nyuma ambapo majira kama haya ya kiangazi kunakuwa hakuna maji ya kutosha.
Mkurugenzi wa SOUWASA mhandisi Patrick Kibasa akizungumzia mipango mikakati inayofanywa na mamlaka hiyo. |
“Tunawashukuru viongozi wa mamlaka ya maji safi na usafi wa Mazingira manispaa ya Songea (SOUWASA) kwa kazi nzuri wanayoifanya na kutufanya sisi akina mama wa majumbani na mama lishe tuweze kufanya kazi zetu za kujitafutia kipato kuwa rahisi ambapo muda wa kwenda umbali mrefu kutafuta maji sisi tunautumia kujitafutia kipato.”amesema Bi. Suzana.
Mmoja wa wenyeviti wa serikali ya mtaa wa Liumbu kata ya Mletele manispaa ya Songea amesema kuwa mtaa wake umeendelea kupata maji licha ya kutangaziwa kutakuwa na mgao kutokana na hali hewa ya ukame.
“Tunampongeza sana Mkurugenzi wa SOUWASA Mhandisi Patrick Kibasa na timu yake kwa kazi nzuri wanayoifanya Kuhakikisha Mji Wetu wa Songea unapata maji muda wote ikilinganishwa na baadhi ya Mikoa ambayo tunaisikia kwenye vyombo vya habari wana matatizo makubwa ya maji.”amesema Kayombo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Generali Wilbert Ibuge amesema kuwa huduma ya maji safi na salama katika Manispaa ya Songea inapatikana kwa asilimia 89.6 ikilinganishwa na asilimia 72.7 kwa mwaka 2020.
Amesema kuwa hali halisi ya upatikanaji wa maji kufikia Juni 2021 watu 1,355,000 walikuwa wanapata huduma ya maji safi na salama kwa Mkoa mzima sawa na asilimia 67.7 kutoka asilimia 62 kwa mwaka 2020 ya wakazi wote wa Mkoa wa Ruvuma ambapo alisema kuwa lengo la Mkoa ni kufikia asilimia 85 kwa wakazi waishio vijijini na 95 kwa wakazi wa mjini ifikapo 2025.
0 Comments