MASHINDANO YA MPIRA WA MIGUU YALIYODHAMINIWA NA KAMPUNI YA MANTRA –NAMTUMBO YAFIKIA TAMATI.


Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma Dr.Julius Ningu akimkabidhi kombe Mchezaji wa timu ya Lucent Fc baada ya kuibuka washindi.

Na Amon Mtega, Namtumbo.

MASHINDANO ya Mpira wa Miguu Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma  yaliyodhaminiwa na Kampuni ya Mantra Tanzania Limited yamefikia tamati huku timu zilizoongoza zimejinyakulia zawadi mbalimbali ikiwemo fedha.

Akihitimisha mashindano hayo ambayo yameenda sambamba na sherehe za miaka 60 ya uhuru wa Tanzania Bara na miaka 59 ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania , mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Dr.Julius Ningu amesema kuwa mashindano hayo yameleta chachu ya kupenda michezo kwa wakazi wa Wilaya hiyo.


Dr.Ningu amesema kuwa mashindano hayo yamefanikiwa vizuri ni kutokana na kampuni ya Mantra Tanzania Limited inayomiliki madini ya Uranium katika mto Mkuju uliopo Wilayani humo kutoa udhamini wa kutosha jambo ambalo limeongeza hamasa ya kutafuta namna ya kuanzisha timu ya Wilaya.

Mkuu huyo ambaye ameipongeza kampuni ya Mantra kwa udhamini huo amesema kuwa ofisi yake inafanya kila mbinu ya kuhakikisha inakuwa na timu ya Wilaya ambayo itakayokuwa inaleta ushindani na timu zingine ikiwemo ya Nje ya Wilaya hiyo.


Mwenyekiti wa Chama Cha mpira wa miguu Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma Zuberi Kossa akizungumzia mafanikio ya mashindano hayo.

Kwa upande wake mwenyekiti wa chama cha mpira wa miguu  Wilayani Namtumbo Zuberi Kossa amesema kuwa mashindano hayo yalishirikisha timu 14 ambazo zote zilipatiwa jezi za kuchezea na kampuni ya Mantra na kuwa timu iliyoibuka mshindi ni timu ya Lucent Fc kwa ushindi wa magoli 2 -0 dhidi ya timu ya Baniani City .

Mwenyekiti Kossa amesema kuwa  zawadi kwa timu hizo  mshindi wa kwanza imejinyakulia  sh.600,000=(Laki sita)Kombe na mpira mmoja,mshindi wa pili Sh.400,000=(Laki nne) na mshindi wa tatu Sh.300,000=(Laki tatu)huku zawadi kwa timu yenye nidhamu itazawadiwa Sh.100,000(Laki moja)ambapo mchezeji bora, mfungaji bora na golikipa bora watapatiwa zawadi Sh.25,000 (Elfu ishirini na tano) kwa kila mmoja.


Kossa ambaye pia ni mratibu wa mashindano ya Kombe la Samia (Samia Cup) amesema kuwa mashindano hayo yameenda sambamba na mashindano ya Kombe la Samia ambayo yameadhimisha siku ya Uhuru wa miaka 60 ya Tanzania bara na miaka 59 ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.


Afisa mahusiano wa Kampuni ya Mantra Tanzania Limited Khadija Pallangyo akizungumzia udhamini uliyofanywa na  Kampuni hiyo.

Naye Meneja mahusiano wa Kampuni ya Mantra Khadija Pallagyo amesema kuwa kampuni hiyo imetoa ufadhili wa fedha Sh.8,000,000=(Milioni Nane) kwaajili ya ununuzi wa vifaa mbalimbali vya michezo ikiwemo jezi kwa timu zote 14 katika mashindano hayo pamoja na kufanikisha kuendesha mashindano hayo.

Meneja mahusiano huyo amesema  kuwa kampuni hiyo imefadhili mashindano hayo ikiwa ni moja ya kuendelea kujenga mahusiano na jamii pamoja kuibua vipaji vya vijana kwa njia za michezo pamoja na kuitangaza Wilaya hiyo.



Pallangyo akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi mwendeshaji na kampuni ya Mantra amesema kuwa kampuni hiyo itaendelea kushirikiana na jamii katika mambo mbalimbali ikiwemo na masuala ya michezo ili kuendana sambamba na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Post a Comment

0 Comments