Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge pamoja na Wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Rufiji wamefika kwenye tukio la moto lililotokea usiku wa kuamkia leo ili kuona athari iliyotokea na jitihada ambazo uongozi wa wilaya wamezichukua kuhakikisha wananchi wanakuwa salama.

Kunenge ametoa pole kwa serikali ya wilaya pamoja na wananchi kwa niaba ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa wote  waliokutwa na madhira hayo na kuwapongeza wakazi wa maeneo ya karibu kuweza kuwapatia hifadhi wananchi wenzao waliokutwa na ajali hiyo na kuwaagiza  uongozi wa wilaya hiyo kufanya haraka kujua tathmini ya athari iliyopatikana ili kuweza kuwasaidia waliopata ajali hiyo.

Nae Mkuu wa wilaya ya Rufiji Meja Edward Gowele akiwa eneo la tukio ameeleza kuwa Moto huo uliotokea mara baada ya mwananchi mmoja aliyefahamika kwa jina la Saba Bakari mwenye umri wa kati ya miaka 30 na 40 akiwa anasafisha eneo lake na kuwasha moto uchafu ndipo moto ulimshinda kwa upepo na kuteketeza nyumba zipatazo 20 za wananchi pamoja na mali na thamani zilizopo ndani ya nyumba hizo na hakuna majeruhi yoyote katika ajali hiyo.

Mkuu huyo wa Wilaya amesema mtuhumiwa amehifadhiwa katika kituo cha polisi jirani kwa ajili ya usalama wake.

 Gowele akitoa taarifa ya awali ya tathimini ndogo asubuhi hii kuwa wamebaini baadhi ya vitu vilivyoungua kuwa ni pamoja na pikipiki moja, baiskeli 5, pesa taslimu zaidi ya shilingi milioni 1, mashine ya kusaga moja.