Kufuatia kukithiri kwa malalamiko katika uendeshaji na utekelezaji wa Mpango wa kunusuru kaya maskini TASAF nchini ,Serikali imelazimika kuja na utaratibu wa kuwasainisha viapo vya uadilifu watendaji wa vijiji na halmashauri zake zenye watu 25 zenye jukumu la kuzitambua na kuzisajili kaya hizo ili kuokoa fedha nyingi ambazo zimekuwa zikitafunwa na watu wasio na sifa baada ya kuingizwa kwenye mpango kimakosa ama kwa kukusudia.
Licha ya changamoto nyingi zinazoripotiwa katika mpango wa TASAF lakini Tangu kuanzishwa kwake 2000 umekuwa na matokeo chanya kwa baadhi ya kaya ambazo zimekuwa zikitumia vyema fedha kidogo inazopata kwa kuanzisha miradi ya kiuchumi ikiwemo Ufugaji na kilimo biashara
Ili kukomesha kabisa changamoto ya wanufaika wasio na sifa na kuzifanya fedha zinazotengwa kuwafikia walengwa ,Zahara Mbailwa amesema serikali imeamua kuanzisha utaratibu wa kusainisha viapo na kisha kuwapa miongozo watendaji wote wa mpango huo ili kusiwepo na upotevu na ubadhilifu wa aina yeyote wa fedha hizo.
"Kutokana na mapungufu makubwa yaliyobainika katika vipindi vya mwanzo serikali imeamua kuanza kusainisha viapo watendaji na wajumbe wa halmashauri kuu za vijiji zenye watu 25 ili kuepusha upendeleo na kuingiza watu wasio na sifa katika mpango"alisema Zahara Mbailwa mwakilishi wa mkurugenzi mkuu wa TASAF makao makuu.
Kwa upande wake muwezeshaji wa mafunzo ya kuwajengea uwezo viongozi ,watendaji na wawezeshaji kuhusu utekelezaji wa mpango wa TASAF kipindi cha pili awamu ya tatu Masejo Songo amesema utakapoanza kufanyika usajili wa wanufaika wapya katika vijiji 28 vilivyoongezwa kwenye mpango watendaji wanapaswa kuzingatia miongozo inayotolewa na serikali ili fedha iwafikie walengwa.
"Tukazingatie taratibu na miongozo iliyotolewa naserikali ili kuwapata wanufaika wa mpango wa awamu ya watatu wenye sifa " Masejo Songo
Awali mkuu wa wilaya ya Makete Juma Sweda ,wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo Viongozi,Watendaji na wawezeshaji amesema awamu zilikuwa na mapungufu makubwa na kusababisha upotevu wa fedha nyingi za serikali na kwamba wakati umefika wa kudhibiti kabisa mnyororo wa wizi.
Sweda amesema tunapaswa kuondoa urafiki ,kujuana na kuingiza siasa katika utekelezaji wa mpango huo ili ukapate mafanikio makubwa ambayo yataongeza ari kwa serikali na wafadhili kuendelea kuzisaidia kaya duni.
"Atakaebainika kufanya vitendo vinavyokwamisha jitihada za serikali za kuzisaidia kaya masikini kwa kuingiza wanufaika wasio na sifa atajikuta katika wakati mgumu mno"Alisema mkuu wa wilaya ya Makete Juma Sweda.
Kwa upande wao washiriki wa mafunzo hayo akiwemo Hawa Kada ambaye ni makamu mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Makete na Jakline Mrosso ambaye ni kaimu mratibu wa TASAF wilaya ya Makete wanasema mafunzo hayo yamewajengea uelewa na uwezo mkubwa katika utekelezaji wa mpango huo huku kitendo cha vijiji 28 kuongezwa kwenye mradi na kuvifanya vijiji vyote vya halmashauri ya wilaya ya Makete vipatavyo 98 kuwa ndani ya mradi.
Akizungumzia awamu ya tatu ya mpango Mrosso amesema awali wilaya hiyo ilikuwa na vijiji 70 tu kati ya 98 katika mpango wa TASAF lakini sasa vijiji vyote vimeingia jambo ambalo litanufaisha familia nyingi duni.
Serikali Imetenga zaidi ya Trioni 3 katika awamu ya tatu ya utekelezaji wa mpango huo.
0 Comments